UWEZESHAJI KIUCHUMI UKEREWE WASHIKA KASI, VIKUNDI 57 VYANUFAIKA NA SH. MILIONI 586.5

UWEZESHAJI KIUCHUMI UKEREWE WASHIKA KASI, VIKUNDI 57 VYANUFAIKA NA SH. MILIONI 586.5

Na Arushadigital | UKEREWE 

Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani imeendelea kuleta matokeo chanya, baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kutoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 586.5 kwa vikundi 57 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mikopo hiyo iliyotolewa Juni 10, 2026 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bukongo, inalenga kuongeza mitaji kwa makundi maalum, kukuza shughuli za uzalishaji mali, kuimarisha ajira za kujitegemea na kuinua uchumi wa kaya za wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, alisema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata fursa za kiuchumi zinazowawezesha kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa mitaji kwa masharti nafuu ili kuwawezesha wananchi kuanzisha na kupanua biashara pamoja na shughuli nyingine za uzalishaji mali.

"Serikali ya Rais Samia imeweka mkazo mkubwa katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Wajibu wetu ni kuhakikisha fursa hizi zinawafikia walengwa na kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao," alisema Ngubiagai.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Vicent Mbua, alisema jumla ya vikundi 57 vilikidhi vigezo na kunufaika na mikopo hiyo yenye thamani ya Sh milioni 586.5.

Alifafanua kuwa awali vikundi 90 viliwasilisha maombi ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2.4, jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Mbua alisema kati ya vikundi vilivyonufaika, vikundi 48 vilipatiwa Sh milioni 444.2 katika awamu ya pili ya utoaji wa mikopo hiyo, huku vikundi vingine tisa vikipokea Sh milioni 142.3, na kufanya jumla ya fedha zilizotolewa kufikia Sh milioni 586.5.

Aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya mikopo hiyo, hatua itakayowezesha wananchi wengi zaidi kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma, alisema vikundi 33 ambavyo vilibainika kuwa na upungufu wa baadhi ya nyaraka na taarifa muhimu vimeelekezwa kufanya marekebisho ili viweze kunufaika katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 unaoanza Julai Mosi.

Mbua pia alisema Serikali itaendelea kutoa elimu na hamasa katika kata ambazo bado hazijawasilisha maombi ya mikopo, zikiwemo Igalla, Mukituntu, Bukiko, Nyamanga, Bwisya na Irugwa, ili wananchi wa maeneo hayo nao waweze kutumia fursa hiyo ya maendeleo.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Wanchoke Chinchibela, alisema usimamizi madhubuti utaendelea kufanyika ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na marejesho yanafanyika kwa wakati.

Alisema usimamizi huo utasaidia mfuko wa mikopo kuendelea kuwa endelevu na kuwafikia wanufaika wengi zaidi katika siku zijazo.

Utoaji wa mikopo hiyo unaendelea kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza maendeleo karibu na wananchi kwa kuwapa fursa za kiuchumi zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi jumuishi na wenye manufaa kwa Watanzania wote.




Ends***

Post a Comment

Previous Post Next Post