LUKUMAY AUNGA MKONO BAJETI KWA ASILIMIA 100, AITAKA SERIKALI KUMALIZA KERO YA BARABARA ARUMERU MAGHARIBI
Na Arusha Digital |DODOMA
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, dkt Johannes Lukumay, ameunga mkono Bajeti Kuu ya Serikali kwa asilimia 100 akisema imejengwa katika msingi wa kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi, huku akiitaka Serikali kuhakikisha changamoto ya miundombinu ya barabara katika jimbo lake inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali bungeni, Dkt. Lukumay alisema bajeti hiyo imeonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutegemea zaidi mapato ya ndani katika kugharamia maendeleo ya nchi.
Alisema hatua ya Serikali kufikia matumizi ya takribani asilimia 70 ya mapato ya ndani katika utekelezaji wa bajeti ni ishara ya kuimarika kwa uchumi wa taifa na uwezo wa kujitegemea katika kufadhili miradi ya maendeleo.
“Bajeti hii ni nzuri, imekaa vizuri na imezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa sababu hiyo naiunga mkono kwa asilimia 100,” alisema Dkt. Lukumay.
Hata hivyo, mbunge huyo alisema pamoja na mafanikio yaliyopo, wananchi wa Arumeru Magharibi bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, hali inayokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Alisema kutokana na Serikali kuongeza fedha katika Mfuko wa Barabara, sasa ni wakati wa kuhakikisha barabara zinazounganisha vijiji na kata mbalimbali za Arumeru Magharibi zinajengwa na kufanyiwa matengenezo ya kudumu.
Dkt. Lukumay alizitaja baadhi ya barabara zinazohitaji kupewa kipaumbele kuwa ni pamoja na barabara za Sokon II–Bangata, Sanawari–Oldonyosambu, Sekei–Olgilai Oltroto–Mlinga, Sambasha–Olamotonyi -Ngaramtoni,Lekamba- Kisongo–Musa, Kilimamoto–Mwandeti, Losinoni Juu–Kisimiri pamoja na Ngoroppo–Emaoi na Maji Moto–Kalangai.
“Wananchi wetu wanahitaji kuona matokeo ya bajeti hii nzuri kupata barabara bora. Miundombinu ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi, biashara, kilimo, utalii na huduma za kijamii. Serikali itumie fursa ya ongezeko la fedha katika Mfuko wa Barabara kutatua changamoto hizi,” alisisitiza.
Katika sekta ya maji, Dkt. Lukumay aliipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa maji katika jimbo lake, akisema utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.
Mbunge huyo pia aliishauri Serikali kuendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuhakikisha Bohari ya Dawa (MSD) inalipwa madeni yake ili iweze kuwa na uwezo wa kununua dawa na vifaa tiba vya kutosha kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini.
Alisema uwekezaji mkubwa katika huduma za afya msingi na vituo vya afya vya karibu na wananchi utasaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuongeza ustawi wa jamii.
Katika hitimisho la mchango wake, Dkt. Lukumay alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake na kwa kusimamia bajeti inayolenga kuimarisha uchumi, huduma za kijamii na maendeleo ya wananchi.
“Tunapoidhinisha bajeti hii, matarajio ya wananchi wa Arumeru Magharibi ni kuona changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi. Kipaumbele chetu kikubwa ni barabara, maji na huduma bora za afya. Haya yakitekelezwa, wananchi wataona thamani ya bajeti hii katika maisha yao ya kila siku,” alisema.
Kauli hiyo ya Dkt. Lukumay imeibua matumaini mapya kwa wananchi wa Arumeru Magharibi wanaotarajia kuona Serikali ikielekeza nguvu zaidi katika kuboresha miundombinu ya barabara ambayo imekuwa kilio cha muda mrefu katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Ends..



Post a Comment