TAASISI YA DINI YA KIISLAMU YA TWARIQATUL QADIRIYA ARRAZIQIYA AL-JAYLANIYA TANZANIA YAHIMIZA MAZUNGUMZO KULINDA AMANI YA TAIFA

 TAASISI YA DINI YA KIISLAMU YA TWARIQATUL QADIRIYA ARRAZIQIYA AL-JAYLANIYA TANZANIA YAHIMIZA MAZUNGUMZO KULINDA AMANI YA TAIFA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA 

TAASISI ya dini ya Kiislamu ya Twariqatul Qadiriya Arraziqiya Al-Jaylaniya Tanzania imewataka Watanzania kuendelea kuilinda amani, umoja na mshikamano wa taifa kwa kutumia mazungumzo, hekima na maridhiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, badala ya kuendekeza vurugu na migogoro inayoweza kuhatarisha maendeleo ya nchi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Sheikh Haruna Husein, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Zawiya Kuu ya Twariqa jijini Arusha.

Sheikh Haruna alisema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na utulivu barani Afrika kutokana na misingi ya umoja, uvumilivu na mshikamano iliyoasisiwa na viongozi wa taifa tangu enzi za waasisi wake, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha tunu hiyo inalindwa na kuendelezwa.

Alisema changamoto na malalamiko yanayowakabili wananchi yanapaswa kujadiliwa kupitia majukwaa halali ya kijamii, kidini na kitaifa ili kupata ufumbuzi wa kudumu unaojenga mshikamano wa wananchi badala ya kuleta migawanyiko.

"Tanzania ni nchi yetu sote. Tunapaswa kutumia njia za mazungumzo, kusikilizana na kuheshimiana katika kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazotukabili. Vurugu hazijawahi kuwa suluhisho la kudumu katika jamii yoyote," alisema Sheikh Haruna.

Alibainisha kuwa mataifa mengi duniani yameendelea kukumbwa na migogoro na machafuko yaliyosababisha hasara kubwa za maisha ya watu, uchumi na mali, jambo linaloonesha umuhimu wa kuimarisha utamaduni wa mazungumzo na maridhiano.

Kwa mujibu wa Sheikh Haruna, Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kuendelea kuwa mfano wa kuigwa duniani kwa kuonesha kwamba tofauti za mawazo na mitazamo zinaweza kushughulikiwa kwa njia za amani bila kuhatarisha utulivu wa taifa.

Aidha, alikumbusha jinsi Watanzania walivyovuka kipindi kigumu cha janga la UVIKO-19 kwa mshikamano na kumtegemea Mwenyezi Mungu, akieleza kuwa changamoto zozote zinazojitokeza zinaweza kushughulikiwa kwa umoja, maombi na ushirikiano.

Katibu Mkuu huyo pia aliwataka waumini wa Twariqa pamoja na waumini wa dini nyingine nchini kuendelea kuiombea Tanzania ili iendelee kuwa nchi ya amani, utulivu na maendeleo.

"Serikali yetu inahitaji dua, ushauri wa kujenga na ushirikiano kutoka kwa wananchi wote. Maendeleo yaliyopatikana kwa miaka mingi yanahitaji kulindwa na kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na taifa lake," alisema.

Alisisitiza kuwa viongozi wa nchi wanapaswa kufikiwa kwa njia za heshima, mazungumzo na hoja zenye kujenga ili mawazo ya wananchi yaweze kusikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi kwa manufaa ya taifa.

Akihitimisha, Sheikh Haruna alisema amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo na kwamba hakuna taifa linaloweza kupiga hatua za kiuchumi na kijamii bila kuwepo kwa utulivu na mshikamano wa wananchi wake.

"Tanzania salama ni jukumu letu sote. Tuendelee kuzungumza, kusikilizana, kuombeana na kushirikiana katika kuijenga Tanzania yenye amani, umoja na maendeleo endelevu," alisema.

Ends. 

Post a Comment

أحدث أقدم