TWAARIQATUL QADIRIYA YATOA WITO WA KULINDA AMANI, YAWATAKA VIJANA KUWA MABALOZI WA UMOJA NA MAENDELEO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
TAASISI ya Kiislamu ya Twariqatul Qadiriya Arraziqiya Al-Jaylaniya Tanzania imewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuzingatia maadili mema kuelekea uchaguzi mkuu na katika safari ya maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Haruna Husein, wakati wa kikao cha kwanza cha Jumuiya ya Vijana wa Twariqatul Qadiriya Arraziqiya Al-Jaylaniya Taifa kilichofanyika katika Zawiya Kuu ya taasisi hiyo jijini Arusha.
Sheikh Haruna alisema amani ni tunu muhimu inayowawezesha wananchi kuishi kwa utulivu, kufanya ibada na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda na kuiendeleza.
“Tunawaomba Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi yetu na kutanguliza amani katika kila jambo. Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani kwa miaka mingi na ni jukumu letu kuhakikisha hali hiyo inaendelea kudumu,” alisema.
Alisisitiza kuwa viongozi wa kisiasa na wananchi wanapaswa kutumia lugha za staha, maridhiano na kuheshimiana badala ya kauli zinazoweza kusababisha migawanyiko na chuki miongoni mwa jamii.
Kwa mujibu wa Sheikh Haruna, taasisi hiyo itaendelea kuhamasisha waumini wake pamoja na jamii kwa ujumla kuzingatia maadili ya dini, upendo na mshikamano ili kuijenga Tanzania yenye umoja, utulivu na maendeleo endelevu.
Akizungumzia nafasi ya vijana katika kulinda amani ya taifa, Sheikh Haruna alisema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani na kuhamasisha maadili mema, huku wakiepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo wakati mwingine imekuwa chanzo cha kusambaza taarifa za uchochezi.
“Tunawajenga vijana wetu katika misingi ya dini, adabu na heshima. Tunataka wawe mfano wa kuigwa katika jamii kwa kuhubiri amani na kuimarisha mshikamano wa kitaifa,” aliongeza.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Twariqatul Qadiriya Arraziqiya Al-Jaylaniya Tanzania, Juma Salimu Juma, aliwataka vijana wa taasisi hiyo nchini kuendelea kudumisha umoja, uzalendo na maadili mema ili wawe chachu ya maendeleo ya jamii na taifa.
Alisema vijana wana nafasi kubwa katika kuendeleza malengo ya taasisi pamoja na kuchangia maendeleo ya nchi, hivyo wanapaswa kutumia nguvu, maarifa na uwezo walionao kwa manufaa ya jamii.
“Vijana ndiyo nguvu ya taasisi yetu na taifa kwa ujumla. Tunapaswa kutumia uwezo tulionao katika kujiletea maendeleo binafsi, kuijenga taasisi yetu na kulitumikia taifa kwa uadilifu na uzalendo,” alisema Juma.
Alisisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kidini huku wakijiepusha na vitendo vinavyoharibu mustakabali wao, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Juma alisema jumuiya hiyo imejipanga kutoa mafunzo na elimu mbalimbali kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kizazi cha sasa na kuwa viongozi bora wa baadaye.
“Tunataka vijana wetu wawe mabalozi wa amani, upendo na mshikamano katika jamii. Tofauti za mitazamo zisivunje umoja wetu, bali zitumike kujenga fikra chanya na maendeleo ya pamoja,” alisema.
Aidha, aliwahimiza wanachama wa jumuiya hiyo kuendeleza ushirikiano, kuheshimu viongozi wa dini na taasisi pamoja na kushiriki kikamilifu katika programu za maendeleo zinazolenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Kwa pamoja, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuendelea kuiombea Tanzania, viongozi wake na wananchi wote ili nchi iendelee kudumisha amani, umoja na utulivu ambao umekuwa msingi wa maendeleo ya taifa kwa miaka mingi.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wanachama wa Jumuiya ya Vijana kueleza dhamira yao ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kidini na maendeleo ya taasisi huku wakiahidi kuwa mabalozi wa amani, mshikamano na maadili mema katika jamii.









إرسال تعليق