SERIKALI YAOMBA AWAMU YA PILI YA MRADI WA MAZIWA FAIDA KUANZA 2027


SERIKALI YAOMBA AWAMU YA PILI YA MRADI WA MAZIWA FAIDA KUANZA 2027

Na Hadija Bagasha | Tanga


Serikali imeomba kuendelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ireland kupitia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Maziwa Faida kuanzia mwaka 2027 hadi 2032, ili kuendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuboresha tija na kuinua kipato cha wafugaji nchini.

Ombi hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Madele, wakati akifungua rasmi Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (TALIRI Open Day 2026) yaliyofanyika katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki jijini Tanga.


Dkt. Madele alisema kuwa Mradi wa Maziwa Faida, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia TALIRI na Taasisi ya Maendeleo ya Kilimo na Chakula ya Ireland (TEAGASC), kwa ufadhili wa Serikali ya Ireland, umeonyesha mafanikio makubwa katika kuleta mageuzi ya kisekta na kuimarisha maisha ya wafugaji, hususan katika Mkoa wa Tanga.

Alieleza kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo, wafugaji wengi walikuwa wakizalisha wastani wa lita tatu hadi tano za maziwa kwa ng’ombe mmoja kwa siku. Hata hivyo, kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji, malisho bora, huduma za ugani zilizoimarishwa na mafunzo kwa wafugaji, uzalishaji umeongezeka hadi wastani wa lita 15 kwa ng’ombe mmoja kwa siku katika maeneo mengi yaliyofikiwa na mradi huo.

“Matokeo haya yanadhihirisha mchango mkubwa wa utafiti, ubunifu na ushirikiano wa maendeleo katika kuongeza tija, kuboresha kipato cha wafugaji na kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini,” alisema Dkt. Madele.

Alisema sekta ya maziwa bado ina fursa kubwa ya kukua kutokana na mahitaji makubwa ya soko la ndani. Kwa sasa Tanzania inazalisha takribani lita bilioni 4.1 za maziwa kwa mwaka, huku mahitaji ya taifa yakikadiriwa kufikia lita bilioni 13 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Dkt. Madele, takwimu hizo zinaonyesha uwepo wa pengo kubwa la uzalishaji ambalo linaweza kuzibwa kupitia uwekezaji zaidi katika teknolojia za kisasa za ufugaji, uzalishaji wa malisho bora na kuimarisha huduma za ugani kwa wafugaji.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Suzanne Keatinge, aliipongeza TALIRI kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kueleza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanaonesha namna ushirikiano wa kimataifa unavyoweza kuleta mabadiliko ya moja kwa moja kwa jamii.

Aliwapongeza watafiti, maafisa ugani, wafugaji na wadau mbalimbali walioshiriki katika utekelezaji wa mradi huo, akisema mchango wao umewezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa tangu kuanzishwa kwa mradi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, alisema mafanikio ya Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Maziwa Faida ulioanza mwaka 2021/2022 na kufikia mwaka 2025/2026, yameweka msingi imara wa kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya maziwa nchini.

Prof. Komba alisema TALIRI itaendelea kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti, ubunifu na teknolojia zinazozalishwa zinawafikia wafugaji wengi zaidi ili kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa sekta hiyo katika soko la ndani na nje ya nchi.

Alibainisha kuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya Euro milioni 3, sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 7 za Kitanzania, umewanufaisha zaidi ya wanawake na vijana 3,000 katika ukanda wa pwani ya mashariki, hususan Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Aidha, alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia mradi huo ni pamoja na kufanya tafiti za malisho bora yanayostahimili mazingira ya ukanda wa pwani, kubaini aina bora za ng’ombe wa maziwa, kuwajengea uwezo maafisa ugani, kutoa mafunzo kwa wafugaji, kuimarisha vyama vya ushirika vya wafugaji na kuboresha miundombinu ya utafiti.

Pia, mradi umeanzisha mashamba darasa yaliyogeuka kuwa vituo muhimu vya mafunzo na usambazaji wa teknolojia za kisasa za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji wa maeneo mbalimbali nchini.

Mradi wa Maziwa Faida sasa unatajwa kuwa miongoni mwa mifano bora ya ushirikiano wa maendeleo unaotumia nguvu ya utafiti, ubunifu na teknolojia katika kukabiliana na changamoto za uzalishaji wa maziwa, huku ukiimarisha mchango wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi.





Post a Comment

Previous Post Next Post