MTOTO ALIYETEKWA TABORA APATIKANA SALAMA, WATUHUMIWA WASHIKILIWA
Na Arushadigital | Tabora
Mwanafunzi wa Darasa la Kwanza katika Shule ya Msingi Bulunde, Kata ya Iborogelo, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Paulina Paul Magushi (6), amepatikana salama baada ya kutoweka kwa zaidi ya wiki moja kufuatia tukio la kutekwa lililoripotiwa Juni 1, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, uchunguzi wa kina uliohusisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama ulifanikisha kubaini mahali alipokuwa mtoto huyo na kumwokoa akiwa hai na salama.
Polisi wameeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mtoto huyo alitekwa na Halima Ramadhan (26), mkazi wa Wilaya ya Nzega, ambaye ni mke wa mjomba wa baba wa mtoto huyo. Baada ya msako mkali uliofanywa na vyombo vya usalama, Paulina alipatikana katika nyumba ya kulala wageni akiwa pamoja na mtuhumiwa huyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya wananchi na vyombo vya dola, huku akibainisha kuwa mtuhumiwa huyo pamoja na mumewe wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira yote ya tukio hili na kuhakikisha wote waliohusika wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria,” alisema Chacha.
Katika mahojiano ya awali na vyombo vya usalama, mtuhumiwa Halima Ramadhan anadaiwa kukiri kuwa alishiriki kumteka mtoto huyo baada ya kutumwa na mumewe, kwa lengo la kudai fedha kutoka kwa familia ya mtoto huyo ili kujipatia kipato.
Akizungumza kwa hisia baada ya kumpokea binti yake, baba mzazi wa mtoto huyo, Paul Magushi Makubi, alisema familia yake ilipokea simu kutoka kwa watu waliodai kuwa wamemteka mtoto huyo na kutaka kulipwa kiasi cha Shilingi milioni 20 kama fidia ili amwachie huru.
“Tulikuwa katika kipindi kigumu sana cha majonzi na hofu. Tunamshukuru Mungu, Serikali na Jeshi la Polisi kwa juhudi zao ambazo zimewezesha mtoto wetu kupatikana akiwa salama,” alisema Makubi.
Naye Diwani wa Kata ya Iborogelo, Emmanuel Bundala, amepongeza kazi iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa, Jeshi la Polisi pamoja na wananchi waliojitokeza kutoa taarifa zilizosaidia kufanikisha operesheni ya kumtafuta mtoto huyo.
Bundala amesema tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa jamii kuendelea kuwa makini na kutoa taarifa kwa haraka wanapobaini vitendo vinavyohatarisha usalama wa watoto, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa watoto katika familia na jamii kwa ujumla.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi wa Igunga na maeneo jirani, huku wengi wakitaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na utekaji huo.
Ends.


