KAMANDA WA POLISI MKOA WA TABORA, SACP RICHARD ABWAO AFARIKI DUNIA
Na Arushadigital
Jeshi la Polisi Tanzania limepata pigo kufuatia kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, ambaye amefariki dunia leo Juni 20, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa za kifo hicho zimethibitishwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime, ambaye amesema Kamanda Abwao alifariki dunia akiwa chini ya uangalizi wa madaktari katika hospitali hiyo ya taifa.
“Ni kweli aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Richard Abwao, amefariki dunia leo Juni 20, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa anapatiwa matibabu,” alisema DCP Misime katika mahojiano na AyoTV.
Kifo cha SACP Abwao kimeacha pengo kubwa ndani ya Jeshi la Polisi na kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora, ambako alikuwa akihudumu kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, akisimamia shughuli za usalama, ulinzi wa raia na mali zao pamoja na utekelezaji wa sheria.
DCP Misime amesema taratibu nyingine zinazohusiana na msiba huo, ikiwemo ratiba za mazishi na shughuli za kuaga mwili wa marehemu, zitatolewa na kutangazwa baadaye na mamlaka husika.
Marehemu SACP Richard Abwao anakumbukwa kwa mchango wake katika kuimarisha usalama, kudhibiti uhalifu na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali aliyowahi kuhudumu nchini.
Taarifa zaidi kuhusu msiba huo zinatarajiwa kutolewa na Jeshi la Polisi Tanzania kadri maandalizi ya mazishi yatakavyoendelea.
Ends.

Post a Comment