UWAJIBIKAJI WAWEKWA MBELE KATIKA BAJETI YA EAC 2026/2027
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania, Machano Ali Machano, amesema uwajibikaji ni nguzo muhimu katika kuhakikisha taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinafanya kazi kwa ufanisi na kufanikisha malengo ya ushirikiano wa kikanda.
Akichangia mjadala wa bajeti ya EAC kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Machano alisema kuwa taasisi za Jumuiya zinapaswa kuimarishwa kwa kupewa rasilimali za kutosha, ikiwemo fedha na watumishi wenye uwezo, ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwajibika kikamilifu kwa wananchi wa Afrika Mashariki.
Alisema bajeti inayopendekezwa inalenga kuongeza uwezo wa kiutendaji wa taasisi za EAC, hatua ambayo itasaidia utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali za maendeleo zinazolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
“Uwajibikaji ni silaha muhimu kwa mafanikio ya taasisi yoyote. Taasisi zikipewa watumishi na fedha za kutosha, zitakuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu yake na kutoa matokeo yanayotarajiwa,” alisema Machano.
Mbunge huyo alibainisha kuwa wabunge wa EALA wamekuwa wakifanya mashauriano na viongozi wa taasisi mbalimbali za EAC, ambapo suala la uwajibikaji limeendelea kupewa kipaumbele kutokana na mchango wake katika kuboresha utendaji wa taasisi hizo na kuongeza tija katika matumizi ya rasilimali za umma.
Aliongeza kuwa Bunge la Afrika Mashariki linatarajia kuidhinisha fedha zilizoombwa na taasisi za Jumuiya kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, likiamini kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.
Machano alisema mafanikio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yatategemea kwa kiwango kikubwa namna taasisi zake zitakavyotumia rasilimali zinazotengwa na jinsi zitakavyowajibika katika kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisisitiza kuwa uwekezaji katika taasisi imara na zinazowajibika ni msingi muhimu wa kufanikisha ajenda ya maendeleo na ushirikiano wa kikanda ndani ya EAC.

Post a Comment