MLAY AKAMATIWA MTWARA BAADA YA KUTOROKA KIFUNGO CHA MIAKA 20 JELA

 TAKUKURU ARUSHA YAMKAMATA MRATIBU WA TASAF ALIYETOROKA HUKUMU YA MIAKA 20 JELA

Na Joseph Ngilisho | Arusha


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imemkamata Amani Elifatio Mlay, aliyekuwa Mratibu wa TASAF katika Jiji la Arusha, baada ya kutoroka hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela aliyopewa na Mahakama kufuatia kutiwa hatiani kwa makosa ya matumizi ya nyaraka za uongo na udanganyifu katika utekelezaji wa mradi wa maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, alisema mshitakiwa huyo alikutwa na hatia tarehe 16 Januari 2026 na Mahakama, baada ya kubainika kuhusika na uwasilishaji wa nyaraka za uongo zilizotumika kumdanganya mwajiri wake katika mchakato wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uzio wa Shule ya Msingi Shangarao.

Ngailo alieleza kuwa katika mwenendo wa kesi hiyo, Mahakama ilithibitisha kuwa mshitakiwa aliandaa na kuwasilisha nyaraka zilizodai kuwa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 64.2 vilikuwa vimepokelewa na kutolewa na mzabuni husika, wakati ukweli ni kwamba hakukuwa na uwasilishaji halisi wa vifaa hivyo.

Alisema baada ya hukumu kutolewa, mshitakiwa alitoroka Mahakamani kabla ya kuanza kutumikia adhabu yake, hali iliyosababisha Mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwake ili kuhakikisha anafikishwa katika mkono wa sheria.

Hata hivyo, Ngailo alisema baada ya ufuatiliaji wa kiintelijensia uliofanywa na TAKUKURU, mtuhumiwa huyo alifanikiwa kukamatwa na kurejeshwa mkoani Arusha kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria na utekelezaji wa hukumu yake.

Alisisitiza kuwa tukio hilo linaonesha dhamira ya taasisi hiyo kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayejificha ili kukwepa mkono wa sheria, akibainisha kuwa TAKUKURU itaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya dola katika kupambana na rushwa na uhalifu wa kiuchumi nchini.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za viashiria vya rushwa na udanganyifu katika miradi ya umma ili kusaidia kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha zinawanufaisha walengwa waliokusudiwa.

Post a Comment

أحدث أقدم