MGOGORO WA ARDHI WACHUKUA SURA MPYA ARUSHA, DALALI ATUNISHA KIFUA ASEMA ASKOFU MONABAN ALIPOTEZA KWA MNADA AKIDAIWA BENK,MONABAN ASISITIZA BADO NI MALI YAKE


MGOGORO WA ARDHI ,ASKOFU MONABAN AIBUA MVUTANO ARUSHA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

Mojaa-Dalali

Mgogoro wa umiliki wa ardhi inayodaiwa kuwa ya Askofu wa Kanisa la KKAM, Philemon Mollel maarufu Monaban, umeendelea kuzua mjadala jijini Arusha baada ya upande unaodai kununua eneo hilo kupitia mnada wa Benki ya CRDB kuendelea na shughuli za maendeleo huku ukisisitiza kuwa unamiliki eneo hilo kihalali.

Suala hilo limeibuka kufuatia madai ya Askofu Monaban kwamba eneo hilo limevamiwa na watu wanaoendelea kufanya shughuli za ujenzi wakati akidai kuwa bado ana haki ya umiliki wa ardhi hiyo.



Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo, Elibariki Mungure maarufu Mojaa, ambaye ni mwakilishi wa upande unaodai kumiliki ardhi hiyo kwa sasa, alisema eneo hilo liliuzwa kwa mnada baada ya Askofu Monaban kushindwa kurejesha mkopo aliouchukua kutoka Benki ya CRDB kwa kutumia ardhi hiyo kama dhamana.

Mojaa alisema mnada huo ulifanyika kwa kufuata taratibu zote za kisheria baada ya tangazo kutolewa kupitia Gazeti la Serikali, na kwamba mnunuzi alilipa zaidi ya Shilingi milioni 400 na kukabidhiwa nyaraka zote muhimu za umiliki.

“Eneo hili halikuvamiwa. Liliuzwa kwa mnada wa kisheria kupitia Benki ya CRDB baada ya mwenye dhamana kushindwa kulipa mkopo. Tunazo nyaraka zote zinazothibitisha umiliki wa sasa wa eneo hili,” alisema Mojaa.

Alieleza kuwa baada ya mnada kukamilika, Askofu Monaban aliwasilisha mashauri mbalimbali mahakamani akipinga mchakato huo, lakini kwa mujibu wa upande wake, hatua hizo hazikubadili umiliki wa eneo hilo.

Mojaa alidai kuwa kwa sasa wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa uwekezaji katika eneo hilo, ikiwemo maandalizi ya ujenzi wa hoteli, huku wakitumia moja ya majengo yaliyopo kama ghala la kuhifadhi vifaa vya ujenzi.

“Tuna hati halali ya umiliki, vibali vya ujenzi na nyaraka zote zinazoturuhusu kuendeleza eneo hili. Kazi zinaendelea kama kawaida na hakuna amri yoyote ya mahakama inayozuia maendeleo yanayofanyika hapa,” alisema.

Aidha, alikanusha madai kwamba eneo hilo linatumika kama kanisa, akisisitiza kuwa kwa sasa linatumika kwa shughuli zinazohusiana na mradi wa maendeleo unaotekelezwa na mmiliki mpya.

Katika maelezo yake, Mojaa pia alidai kuwa Askofu Monaban amekuwa akiwasilisha malalamiko kwa mamlaka mbalimbali za serikali ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha akitaka shughuli za ujenzi zisitishwe, lakini akasema upande wao uko tayari kuwasilisha nyaraka zote zinazothibitisha umiliki wao mbele ya mamlaka husika.

Alisema eneo hilo lilikuwa dhamana ya mkopo uliochukuliwa na Askofu Monaban katika Benki ya CRDB na kwamba baada ya kushindwa kulipa deni hilo, benki ilitumia mamlaka yake ya kisheria kuuza mali hiyo kupitia mnada wa wazi.

Kwa mujibu wa Mojaa, mnunuzi wa eneo hilo alikamilisha malipo yote yaliyohitajika na baadaye akapatiwa hati pamoja na nyaraka nyingine za umiliki, jambo ambalo linawapa haki ya kuendelea na matumizi ya ardhi hiyo.

Askofu MONABAN

Hata hivyo, Askofu Philemon Mollel maarufu Monaban ameendelea kusisitiza kuwa eneo hilo ni mali yake na amekuwa akipinga hatua za maendeleo zinazoendelea kufanyika katika eneo hilo huku akitaka mamlaka za serikali na vyombo vya sheria kuingilia kati.

Wakati huo huo, mamlaka za serikali zimeelezwa kuendelea kufuatilia suala hilo huku zikisubiri nyaraka na vielelezo kutoka pande zote mbili kabla ya kutoa maelekezo au maamuzi yoyote kuhusu hatma ya eneo hilo.

Mgogoro huo unaendelea kuvuta hisia za wananchi wa Arusha huku kila upande ukisisitiza kuwa una nyaraka halali zinazounga mkono madai yake ya umiliki wa ardhi hiyo.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post