LUKUMAY ACHARUKA, AIBANA SERIKALI BUNGENI KUHUSU BILIONI 3 ZA MRADI WA MAJI OLDONYOSAMBU

LUKUMAY AIBANA SERIKALI KUHUSU MRADI WA MAJI OLDONYOSAMBU ULIOKWAMA

By Arushadigital|DODOMA

MBUNGE  wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameibana Serikali kueleza ni lini itatoa fedha zilizobaki kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Maji wa Kata ya Oldonyosambu wenye thamani ya shilingi bilioni 6, ambao kwa sasa utekelezaji wake umesimama licha ya kufikia asilimia 52.

Dkt. Lukumay alitoa hoja hiyo bungeni alipouliza swali la nyongeza akitaka kujua hatma ya mradi huo ambao Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 3, huku kiasi kingine cha shilingi bilioni 3 kikiwa bado hakijalipwa kwa mkandarasi.

Alisema kusimama kwa mradi huo kunawaathiri wananchi wa Oldonyosambu ambao wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata huduma ya maji safi na salama, huku changamoto ya upatikanaji wa maji ikiendelea katika maeneo hayo.

“Mradi huu una thamani ya shilingi bilioni 6. Serikali imelipa shilingi bilioni 3 na bado kuna shilingi bilioni 3 ambazo mkandarasi anapaswa kulipwa. Kwa sasa mradi umefikia asilimia 52 ya utekelezaji lakini umesimama. Serikali ituambie ni lini fedha zilizobaki zitapelekwa ili wananchi wa Oldonyosambu wapate huduma hii muhimu,” alihoji Dkt. Lukumay.

Akijibu swali hilo bungeni, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, alisema Serikali inafahamu changamoto ya kusimama kwa Mradi wa Maji wa Oldonyosambu na kutambua umuhimu wake kwa wananchi wa Arumeru Magharibi.

Alisema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 6 tayari umefikia asilimia 52 ya utekelezaji wake, huku mkandarasi akisubiri kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 3 zilizobaki ili kuendelea na kazi za ujenzi.

Kundo alisema Serikali imeuweka mradi huo katika kipaumbele na kwamba fedha zitakapopatikana zitaelekezwa moja kwa moja kwa mkandarasi ili kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika na wananchi wanaanza kupata huduma ya maji safi na salama.

“Ni moja ya miradi tunayoifuatilia kwa karibu kutokana na umuhimu wake. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mradi huu unakamilika ili kuondoa changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Oldonyosambu na maeneo jirani,” alisema Kundo.

Aidha, Serikali ilisisitiza kuwa itaendelea kutoa kipaumbele kwa miradi ya maji yenye manufaa makubwa kwa wananchi ili kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu nchini.

Ends...

Post a Comment

Previous Post Next Post