KAYOMBO AWAPIGA SUTI NZITO MADEREVA 30 WA JIJI LA ARUSHA , ATAKA WATUMISHI WAPENDEZE KAZINI KAMA YEYE!

KAYOMBO AWAPIGA SUTI NZITO MADEREVA 30 WA JIJI LA ARUSHA , ATAKA WATUMISHI WAPENDEZE KAZINI KAMA YEYE!

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA

MKURUGENZI wa Jiji la Arusha, John Kayombo, ameanzisha mpango wa kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa jiji hilo kwa kuwapatia suti mbili kila mmoja madereva 30 wa jiji pamoja na watumishi wa kitengo cha usafiri, hatua inayolenga kuimarisha nidhamu, hadhi ya kazi na mwonekano wa watumishi hao wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mavazi hayo katika jiji hilo Juni 26,2026, Kayombo alisema ni muhimu kwa watumishi wa umma kuendana na hadhi ya taasisi wanazozihudumia kwa kuwa na mwonekano unaovutia na unaoakisi heshima ya kazi wanayoifanya.

Alisema jiji limeendelea kuboresha huduma kwa kununua magari mapya ya kisasa, hivyo ni jambo lisilokubalika kuona dereva wa gari la serikali akiwa amevaa mavazi yasiyoendana na hadhi ya kazi yake.

“Tuna magari mapya na ya kisasa, lakini wakati mwingine unakutana na dereva ameendesha gari jipya huku amevaa ovyo. Hilo halileti picha nzuri ya taasisi. Ndiyo maana tumeamua kuwashonea suti madereva wote ili waonekane nadhifu na wenye hadhi,” alisema Kayombo.

Alifafanua kuwa katika awamu ya kwanza kila dereva amepewa suti mbili, huku utaratibu ukiwekwa wa kuhakikisha kila mwaka watumishi hao wanapatiwa mavazi mapya ili kuendeleza mwonekano mzuri na kuongeza morali ya kazi.

Kwa mujibu wa Kayombo, madereva wa Jiji la Arusha watakuwa na utaratibu maalumu wa kuvaa suti kwa siku maalumu za kazi kila wiki, jambo litakalowatofautisha na madereva wa mamlaka nyingine nchini.

“Tunataka ukimuona dereva wa Jiji la Arusha uweze kumtofautisha na dereva wa taasisi nyingine yoyote Tanzania. Tunajenga utamaduni wa nidhamu, umoja na mwonekano wa kitaalamu,” alisisitiza.

Mbali na madereva, Kayombo alisema mpango huo utaendelea kuwafikia watumishi wengine wa jiji kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kazi yatakayowafanya wajisikie kuthaminiwa na mwajiri wao.

Alieleza kuwa watumishi wanapopewa mazingira mazuri ya kazi, huongeza ari ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya taasisi.

“Nataka Arusha ya kisasa, Arusha ambayo watumishi wanaishi na kufanya kazi kama familia moja. Mfanyakazi akifika kazini ajisikie yupo mahali salama na anathaminiwa. Hilo linaongeza uwajibikaji na ufanisi,” alisema.

Kayombo aliongeza kuwa mageuzi anayoyalenga ndani ya Jiji la Arusha hayataishia kwenye miundombinu na huduma pekee, bali yatahusisha pia ustawi wa watumishi, nidhamu ya kazi na kujenga taswira bora ya taasisi mbele ya wananchi.

Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na madereva wa jiji hilo ambao wameeleza kuwa itawapa motisha zaidi ya kufanya kazi kwa bidii huku wakiwakilisha vyema sura ya Jiji la Arusha mbele ya wananchi na viongozi wanaowahudumia.


Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post