KANGA GALA KUTIKISA ARUSHA JUNI 19,WADAU KUITIZAMA AFYA YA AKILI KWA WANAWAKE KWA KINA, FURSA ZA KIUCHUMI PIA ZITAKUWEPO

KANGA GHALA YAKUSANYA WADAU KUJADILI CHANGAMOTO ZA AFYA YA AKILI KWA WANAWAKE ARUSHA

Na Joseph Ngilisho |ARUSHA

JUKWAA la Kanga Ghala 2026 litakalojumuisha mamia ya wanawake ndani na nje ya Mkoa wa Arusha linatarajiwa kufanyika Juni 19, 2026 katika Jengo la OTTU (Business Center) jijini Arusha, likiwa na lengo la kuibua mjadala mpana kuhusu changamoto za afya ya akili zinazoikabili jamii, hususan wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mratibu wa kongamano hilo, Jane Edward, alisema Kanga Ghala ni jukwaa maalumu linalotumia kanga kama alama ya utamaduni, umoja na utambulisho wa mwanamke wa Kitanzania, huku likitoa nafasi ya kujadili masuala muhimu ya kijamii na kiuchumi yanayogusa maisha ya wanawake.

Jane alisema changamoto za afya ya akili zimeendelea kuongezeka kutokana na shinikizo la maisha, majukumu ya kifamilia, mazingira ya kijamii na changamoto za kiuchumi, hali inayowafanya wanawake wengi kukumbwa na msongo wa mawazo bila kupata nafasi ya wazi ya kuzungumza.

“Afya ya akili imekuwa changamoto kubwa katika jamii yetu. Wanawake wengi wanapitia msongo wa mawazo na matatizo mbalimbali bila kupata msaada wa kutosha au nafasi ya kueleza changamoto zao,” alisema Jane.

Alisema kupitia kongamano hilo, washiriki watapata fursa ya kusikiliza mada kutoka kwa wataalamu wa afya ya akili, kujifunza namna ya kutambua dalili za mapema na kupata mbinu za kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa mujibu wake, kongamano hilo pia litajumuisha huduma mbalimbali za afya ikiwemo uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, elimu ya afya ya uzazi na ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu, sambamba na maonesho ya kanga, burudani za kitamaduni na shughuli za kijamii zitakazolenga kuimarisha mshikamano wa wanawake.

Jane alitoa wito kwa wanawake, vijana na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo ili kupata elimu itakayosaidia kuboresha afya ya akili na ustawi wa jamii kwa ujumla.

“Tunataka jamii inayoweza kuzungumza kwa uwazi kuhusu afya ya akili bila hofu wala unyanyapaa. Kanga Ghala ni jukwaa la kuelimisha, kuhamasisha na kuunganisha jamii,” alisisitiza.

Muuguzi na Tabibu wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, Magreth Msigwa, alisema kongamano hilo ni jukwaa muhimu litakalosaidia kuongeza uelewa wa afya ya akili kwa wanawake na jamii kwa ujumla.

Msigwa alisema wanawake ndio kundi linaloathirika zaidi, akibainisha kuwa takwimu zinaonyesha kati ya asilimia 50 hadi 57 ya wanawake hukumbwa na changamoto za afya ya akili katika hatua mbalimbali za maisha yao.

Alisema hali hiyo husababishwa na msongo wa mawazo, changamoto za kiuchumi, majukumu ya kifamilia pamoja na ukatili wa kijinsia.

“Kupitia Kanga Ghala tunapata nafasi ya kutoa elimu ya afya ya akili, kuwasaidia watu kutambua dalili za mapema na namna ya kukabiliana nazo kabla hazijawa kubwa,” alisema Msigwa.

Alisisitiza kuwa afya ya akili ni msingi wa ustawi wa mtu binafsi, familia na maendeleo ya jamii, akiwataka wanawake kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo.

Kongamano hilo limeendelea kupata uungwaji mkono kutoka kwa taasisi mbalimbali zikiwemo sekta binafsi na mashirika ya kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Voice of Women Africa, Veronica Kidemi, alisema ameguswa na ajenda ya afya ya akili kutokana na uzoefu wake binafsi baada ya kupoteza mkono wake wa kulia kufuatia ukatili mwaka 2020, hali iliyomuweka katika changamoto za kisaikolojia.

Alisema kupitia uzoefu huo, alianzisha taasisi yake ili kuhamasisha wanawake kujikubali na kutafuta msaada wa afya ya akili badala ya kukata tamaa.

“Nilipitia changamoto kubwa za kihisia na kisaikolojia, lakini nilijifunza kuzibadilisha kuwa nguvu ya kusonga mbele,” alisema Kidemi.

Alisisitiza wanaume kuwasaidia wake zao kushiriki kongamano hilo ili kupata elimu itakayosaidia kuimarisha familia na jamii kwa ujumla.

Benki ya Azania pia imetangaza kuunga mkono kongamano hilo, ambapo Afisa Mahusiano Winfrida Mwacha alisema taasisi hiyo inaendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia elimu ya fedha na mikopo yenye masharti nafuu.

Alisema uwezeshaji wa kiuchumi unachangia kupunguza msongo wa mawazo na kuboresha afya ya akili.

“Tunamuwezesha mwanamke ili aweze kujitegemea kiuchumi, na hivyo kuchangia ustawi wa familia na jamii,” alisema Mwacha.

Kwa upande wa Hoteli ya Four Point Sheraton Arusha nayo imethibitisha kushiriki katika kongamano hilo, ambapo mfanyakazi wake Jacqueline Joel alisema taasisi hiyo inaunga mkono juhudi za kuongeza uelewa wa afya ya akili.

Alisema kongamano hilo litatoa nafasi kwa wanawake kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kijamii na kikazi.

Kongamano la Kanga Ghala 2026 linatarajiwa kuwa moja ya majukwaa makubwa ya kijamii na kielimu jijini Arusha, likileta pamoja wataalamu, taasisi na wananchi kujadili na kutafuta suluhisho la changamoto za afya ya akili, hususan kwa wanawake.



***Ends***

Post a Comment

أحدث أقدم