JKT YATOA FURSA YA MWISHO KWA VIJANA WALIOSHINDWA KURIPOTI MAKAMBINI
Na Moreen Rojas| DODOMA
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetoa fursa ya mwisho kwa vijana waliohitimu Kidato cha Sita mwaka 2026 na kuchaguliwa kujiunga na Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria, lakini hawakufanikiwa kuripoti katika makambi waliopangiwa awali, kwa kuwataka kuripoti katika makambi yaliyo karibu na maeneo wanayoishi kuanzia Juni 12 hadi 15, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 12, 2026, katika Makao Makuu ya JKT yaliyopo Chamwino jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Operesheni na Mafunzo wa JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, alisema hatua hiyo inatekeleza maelekezo ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele, ya kuhakikisha vijana wote waliochaguliwa wanapata fursa ya kushiriki mafunzo hayo muhimu kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
Alisema awali vijana hao walitakiwa kuripoti katika makambi waliopangiwa kuanzia Juni 1 hadi 7, 2026, lakini baadhi yao walishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali.
“Baada ya kutathmini hali hiyo, Mkuu wa JKT ameagiza vijana wote ambao bado hawajaripoti kuruhusiwa kwenda katika makambi ya JKT yaliyo karibu na maeneo wanayoishi ili kuendelea na taratibu za kujiunga na mafunzo hayo,” alisema Brigedia Jenerali Mnyani.
Alifafanua kuwa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria yana lengo la kuwajengea vijana uzalendo, nidhamu, uzingatiaji wa sheria, stadi za maisha pamoja na kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na ujenzi wa taifa.
Hata hivyo, alibainisha kuwa utaratibu huo wa kuripoti katika makambi ya karibu hautahusisha Kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani, Kambi ya Makutupora JKT mkoani Dodoma pamoja na Chuo cha Uongozi cha JKT (CUJKT) kilichopo Kimbiji jijini Dar es Salaam.
Aidha, JKT limewataka vijana wote ambao bado hawajatekeleza wito huo kuhakikisha wanaripoti katika makambi husika kati ya Juni 12 na Juni 15, 2026, kwani hiyo ndiyo fursa ya mwisho iliyotolewa kabla ya hatua nyingine za kiutawala kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Jeshi la Kujenga Taifa.
Jeshi hilo limewahimiza vijana waliochaguliwa kutumia nafasi hiyo muhimu kwa manufaa ya maendeleo yao, huku likisisitiza kuwa mafunzo ya JKT yana mchango mkubwa katika kuandaa nguvu kazi yenye uzalendo, nidhamu na uwajibikaji kwa taifa.
Ends..




