HANNY G INVESTMENT YAJIVUNIA KUZIFIKIA TAASISI ZAIDI YA 700 KUPITIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
KAMPUNI ya Hanny G Investment yenye makao yake Kiseliani-Moshono katika Jiji la Arusha imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, ambapo imefanikiwa kuzifikia taasisi zaidi ya 700 kupitia huduma zake za uzalishaji na usambazaji wa majiko pamoja na nishati mbadala ya kupikia.
Akizungumza kuhusu shughuli za kampuni hiyo katika kongamano la nishati lililofunguliwa na Naibu waziri wa Nishati,Salome Nakamba jijini Arusha, Meneja Masoko wa Hanny G Investment, Zera Negro, amesema kampuni imejikita katika utengenezaji wa majiko ya kisasa yanayotumia umeme, gesi na briquettes zinazotokana na mabaki ya mazao ya kilimo, kwa lengo la kutoa suluhisho endelevu la nishati kwa taasisi na kaya.
Amesema mafanikio ya kampuni hiyo yameiwezesha kufikia taasisi zaidi ya 700 nchini zikiwemo shule, hospitali, magereza, vyuo, taasisi za kidini na ofisi mbalimbali zinazohudumia idadi kubwa ya wananchi kila siku.
“Tunajivunia kuona kuwa kupitia kampeni za uhamasishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia, tumefanikiwa kuzifikia taasisi zaidi ya 700 nchini. Hii ni hatua kubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema Zera.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo imewekeza katika teknolojia za kisasa zinazosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, huku zikilinda afya za watumiaji na mazingira.
Kwa mujibu wa Zera, briquettes zinazozalishwa na Hanny G Investment hutengenezwa kutokana na mabaki ya mazao ya kilimo yanayopatikana ndani ya nchi, jambo linalosaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na wakati huo huo kupunguza utegemezi wa rasilimali za misitu.
Amesema mbali na kusambaza bidhaa zake, kampuni imekuwa ikitoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi mbalimbali nchini, huku ikifanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha wateja wanaendelea kunufaika na huduma hizo.
“Tunatoa elimu kuhusu faida za nishati safi ya kupikia, namna ya kuitumia kwa ufanisi na umuhimu wake katika kulinda afya za wapishi pamoja na mazingira. Pia tunafanya ufuatiliaji kuhakikisha taasisi zinaendelea kupata manufaa yaliyokusudiwa,” amesema.
Amebainisha kuwa matumizi ya majiko yanayotumia nishati safi hupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi, huongeza ufanisi wa upishi na kuondoa changamoto za moshi ambazo mara nyingi husababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
Aidha, amesema Hanny G Investment itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kusaidia kufikiwa kwa lengo la Taifa la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Tunao wajibu wa kuhakikisha jamii inaelewa faida za nishati safi na inashiriki kikamilifu katika matumizi yake. Hii siyo tu kwa ajili ya kupika, bali ni uwekezaji katika afya, mazingira na maendeleo ya uchumi wa Taifa,” amesema.
Ends..








