FEAJ YAWEKA MIKAKATI YA KUINUA TASNIA YA HABARI AFRIKA MASHARIKI

FEAJ YAWEKA MIKAKATI YA KUINUA TASNIA YA HABARI AFRIKA MASHARIKI

Na Arushadigital | Mombasa

Shirikisho la Waandishi wa Habari Ukanda wa Afrika Mashariki (FEAJ) limefanya mkutano wake maalum wa kwanza tangu viongozi wake wachaguliwe mwaka jana, likilenga kuweka mikakati ya kuimarisha tasnia ya habari na kutatua changamoto zinazowakabili wanahabari katika nchi za ukanda huo.

Akifungua mkutano huo uliofanyika Juni 20, 2026 mjini Mombasa, Rais wa FEAJ, Erick Oduor, alisema shirikisho hilo limejipanga kuwa jukwaa la kuwaunganisha wanahabari wa Afrika Mashariki ili kufanya kazi kwa pamoja na kutafuta suluhu za changamoto zinazofanana katika sekta ya habari.

Oduor alisema kuwa mazingira ya kazi za uandishi wa habari katika nchi nyingi za Afrika Mashariki yanafanana, jambo linalohitaji kuwepo kwa mikakati ya kikanda itakayosaidia kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa wanahabari na maendeleo ya taaluma hiyo.

Aliongeza kuwa FEAJ imekusudia kuanzisha miradi mbalimbali ya kikanda itakayosaidia kuboresha uwezo wa wanahabari, kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kuongeza uzalishaji wa habari zenye manufaa kwa wananchi wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ), Omar Faruk Osman, aliwataka wanahabari wa ukanda huo kuwaunga mkono viongozi wa FEAJ ili kufanikisha dhamira ya kuimarisha sekta ya habari.

Osman alisema FAJ itaendelea kushirikiana na FEAJ katika kutetea uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa wanahabari na ustawi wa vyama vya wanahabari katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.

"Waungeni mkono viongozi wa FEAJ ili kuimarisha tasnia ya habari katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Sisi FAJ tutaendelea kuwapa ushirikiano na msaada unaohitajika," alisema Osman.

Naye Katibu Mkuu wa FEAJ, Solange Ayanone, alisema shirikisho hilo linatarajia kuanzisha programu mbalimbali za kuzijengea uwezo taasisi na vyama vya wanahabari ili viweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Viongozi waliochaguliwa kuongoza FEAJ kwa kipindi cha miaka mitano ni Erick Oduor wa Chama cha Waandishi wa Habari Kenya (KUJ) akiwa Rais, Patrick Oyet wa Chama cha Waandishi wa Habari Sudan Kusini akiwa Makamu wa Rais na Solange Ayanone kutoka Rwanda akiwa Katibu Mkuu. Wajumbe wa Kamati Kuu ni Mussa Juma wa JOWUTA Tanzania pamoja na Promise Twinamukye kutoka Uganda.

Kabla ya mkutano huo, viongozi na wanachama wa FEAJ walihudhuria warsha ya siku tatu kuhusu masuala ya wahamaji na fursa zinazopatikana kwao. Warsha hiyo ilifadhiliwa na International Labour Organization pamoja na wadau wengine, na iliwakutanisha viongozi wa vyama vya wanahabari kutoka Comoro, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.



Ends .

Post a Comment

Previous Post Next Post