DCEA KANDA YA KASKAZINI YAKAMATA WATUHUMIWA 550 WA DAWA ZA KULEVYA KWA MWAKA MMOJA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini imefanikiwa kukamata watuhumiwa 550 wa makosa mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, huku ikitekeleza operesheni 227 katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Akisoma taarifa hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya yaliyofanyika katika Kanisa la Selian Community Church jijini Arusha, Afisa Ustawi wa Jamii wa DCEA Kanda ya Kaskazini, Brenda Mbati, alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya DCEA, vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi mbalimbali na wananchi katika kutoa taarifa na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya, huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya watuhumiwa waliokamatwa, wanaume walikuwa 442 na wanawake 108, huku kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kikikamatwa katika operesheni mbalimbali zilizofanyika ndani ya mwaka mmoja.
Jumla ya kilo 5,417.26 za mirungi, kilo 3,010.30 za bangi na gramu 14 za heroin zilikamatwa katika mikoa yote minne ya kanda hiyo.
Mkoa wa Arusha uliongoza kwa idadi ya operesheni na watuhumiwa waliokamatwa ambapo operesheni 121 zilifanyika na kusababisha kukamatwa kwa watuhumiwa 413, wakiwemo wanaume 338 na wanawake 75. Mkoa huo pia ulikamata kilo 1,458.26 za mirungi na kilo 2,977.03 za bangi.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro, operesheni 50 zilifanyika na watuhumiwa 72 kukamatwa, huku kilo 1,568.61 za mirungi na kilo 13.02 za bangi zikikamatwa.
Mkoa wa Tanga ulifanya operesheni 49 na kukamata watuhumiwa 33, wakiwemo wanaume 30 na wanawake watatu. Katika operesheni hizo, kilo 1,814.49 za mirungi, kilo 20.25 za bangi na gramu 14 za heroin zilikamatwa.
Aidha, pikipiki 50 zilizokuwa zikitumika kusafirisha mirungi zilikamatwa mkoani Tanga. Watuhumiwa 19 walikamatwa kuhusiana na matukio hayo ambapo saba walinyimwa dhamana na kufikishwa mahakamani huku 12 wakipewa dhamana.
Katika Mkoa wa Manyara, operesheni saba zilifanyika na kusababisha kukamatwa kwa watuhumiwa 32, wakiwemo wanaume 24 na wanawake wanane, huku kilo 575.90 za mirungi zikikamatwa.
Mbali na ukamataji huo, watuhumiwa wanne katika kesi tatu tofauti walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Mkinga kwa makosa yanayohusiana na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika kipindi hicho, DCEA kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilifungua na kufuatilia kesi mbalimbali katika mikoa yote ya kanda hiyo. Jumla ya watuhumiwa 10 walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, wawili walihukumiwa miaka minne jela kwa biashara ya dawa za kulevya, huku mmoja akihukumiwa kifungo cha miaka mitano.
Pia, watuhumiwa 11 walikutwa na hatia ya matumizi ya dawa za kulevya na kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja, wakati saba walipatiwa adhabu ya kifungo cha nje na kufanya kazi za kijamii chini ya uangalizi kwa miaka mitatu.
Mbali na operesheni za ukamataji, DCEA Kanda ya Kaskazini imeendelea kuwekeza katika elimu kwa jamii ambapo wananchi 136,132 walifikishwa na kupewa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya katika kipindi hicho.
Elimu hiyo iliwahusisha wanafunzi, viongozi wa dini na kimila, vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za serikali na binafsi, waendesha bodaboda, wanawake wajawazito, watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani pamoja na makundi mengine mbalimbali ya kijamii.
Katika upande wa huduma za matibabu na urejeshaji wa waraibu, DCEA imeendelea kushirikiana na nyumba 32 za upataji nafuu katika kanda hiyo ambazo zinahudumia waraibu 937. Vituo vya MAT vya Hospitali ya Bombo Tanga, Hospitali ya Mount Meru na Kituo cha Afya Ubwari Muheza vinaendelea kutoa huduma kwa wagonjwa 771 wanaopata nafuu, huku watu 325 wakimaliza matibabu yao kwa mafanikio.
Kwa kushirikiana na mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSSSF na NSSF, DCEA pia imefanikiwa kugawa vitanda 160 na magodoro 160 katika nyumba 19 za upataji nafuu mkoani Arusha ili kuboresha mazingira ya huduma kwa waraibu wanaoendelea na matibabu.
Mbati alisema maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Ubunifu wa Kimkakati: Suluhisho la Changamoto za Dawa za Kulevya,” ambayo inalenga kuhamasisha matumizi ya mbinu mpya, ushirikiano wa wadau na ubunifu katika kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na DCEA pamoja na vyombo vingine vya dola kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya ili kuimarisha usalama wa jamii na kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya athari za matumizi na biashara haramu ya dawa hizo.
Ends .








إرسال تعليق