BALOZI MATINYI AKABIDHI HATI ZA UTAMBULISHO ALGERIA, AAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI
Na Arushadigital | Algiers-Algeria
Balozi mpya wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, amekabidhi rasmi hati zake za utambulisho kwa Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Algiers Juni 10, 2026, hatua inayompa mamlaka ya kuanza kutekeleza majukumu yake ya kidiplomasia nchini humo.
Katika mazungumzo yaliyofanyika mara baada ya hafla hiyo, Balozi Matinyi alimfikishia Rais Tebboune salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na kutoa shukrani kwa Serikali na wananchi wa Algeria kwa kuendeleza uhusiano wa kihistoria na wa kindugu kati ya mataifa hayo mawili ambao umeendelea kudumu kwa zaidi ya miaka 60.
Balozi Matinyi alisema Tanzania na Algeria zimepiga hatua kubwa katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano, hususan sekta za ulinzi na elimu ya juu, na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kupanua ushirikiano huo katika nyanja za uchumi na maendeleo ili wananchi wa nchi zote mbili waweze kunufaika zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na Rais Tebboune, Balozi Matinyi alisema viongozi hao walijadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati zikiwemo kilimo, viwanda, utengenezaji wa dawa, nishati, madini na utalii.
Aidha, alisema pande hizo mbili zimeonyesha dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya sayansi, teknolojia, utafiti, utamaduni, elimu ya juu pamoja na ulinzi, kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya watu kwa watu na kukuza maendeleo ya pamoja.
“Nimepewa jukumu na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria unaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa mataifa yetu mawili. Kwa kutumia maono na uongozi wa viongozi wetu, ninaamini tutafanikisha malengo hayo,” alisema Balozi Matinyi.
Kwa upande wake, Rais Tebboune alieleza utayari wa Algeria kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo na uchumi. Alisisitiza kuwa serikali yake iko tayari kuendeleza majadiliano na kufikia makubaliano mapya yatakayoongeza fursa za ushirikiano kupitia vikao vya pamoja vya serikali na ziara za viongozi wa ngazi mbalimbali.
Wachambuzi wa masuala ya diplomasia wanaeleza kuwa hatua hiyo inaashiria mwanzo mpya wa kuimarika kwa mahusiano ya Tanzania na Algeria, hasa katika kipindi ambacho nchi za Afrika zinaendelea kuhamasisha biashara ya ndani ya bara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kupitia makubaliano ya eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA).
Balozi Matinyi anakuwa balozi wa nne kuiwakilisha Tanzania nchini Algeria tangu kufunguliwa kwa ubalozi huo. Amewafuata mabalozi waliomtangulia ambao ni Omari Yussuf Mzee (2017–2020), Meja Jenerali Jacob Kingu (2020–2023) na Imani Njalikai (2023–2026).
Mbali na kuiwakilisha Tanzania nchini Algeria, Ubalozi wa Tanzania uliopo Algiers pia unasimamia mahusiano ya kidiplomasia katika nchi za Tunisia, Mauritania, Niger pamoja na Sahrawi Arab Democratic Republic.
Hafla ya kukabidhi hati za utambulisho imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria, huku matarajio makubwa yakielekezwa katika kuongeza biashara, uwekezaji na kubadilishana utaalamu katika sekta mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo mawili.
