BALTON TANZANIA YAZINDUA VIUATILIFU 10 VIPYA KUKABILIANA NA WADUDU NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI
Na Arushadigital|MWANZA
Kampuni ya Balton Tanzania Ltd imezindua viuatilifu 10 vipya vyenye teknolojia ya kisasa vinavyolenga kuwasaidia wakulima wa mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga, mahindi, kahawa, korosho, nyanya, vitunguu na maharage kukabiliana na wadudu waharibifu, magugu vamizi pamoja na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Uzinduzi wa viuatilifu hivyo umefanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane jijini Mwanza, ukihusisha wafanyabiashara wakubwa wa pembejeo na viuatilifu kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu, Tabora na Kigoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja Mkuu wa Balton Tanzania Ltd, Jacob Vorster, alisema bidhaa hizo mpya ni hatua muhimu ya kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuwapatia wakulima suluhisho la kisasa litakalowawezesha kuongeza uzalishaji na kupata mavuno bora.
Alisema viuatilifu hivyo vimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu inayosaidia kudhibiti usugu wa wadudu waharibifu pamoja na kuangamiza magugu yanayoathiri ukuaji wa mazao.
“Bidhaa hizi zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wakulima wa Tanzania. Lengo letu ni kuwasaidia kupata mavuno mengi na yenye ubora huku wakikabiliana kwa ufanisi na changamoto za wadudu na magugu,” alisema Vorster.
Aliwahimiza wakulima kununua viuatilifu hivyo kupitia maduka rasmi ya pembejeo za kilimo yaliyoidhinishwa nchini ili kuhakikisha wanapata bidhaa zenye ubora na usalama unaotakiwa.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Sayansi ya Mimea wa Balton Tanzania, Chonya Wema, alisema viuatilifu hivyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazozikabili sekta za kilimo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alibainisha kuwa ongezeko la wadudu waharibifu na magugu vamizi limekuwa tishio kwa uzalishaji wa mazao katika maeneo mengi nchini, hivyo bidhaa hizo zitasaidia kuongeza tija kwa wakulima.
“Tunafahamu athari kubwa zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi katika uzalishaji wa mazao. Balton imekuja na suluhisho la kisasa litakalosaidia kudhibiti wadudu waharibifu pamoja na magugu vamizi yanayopunguza uzalishaji mashambani,” alisema.
Aidha, alisema kampuni hiyo imeweka mtandao mpana wa mawakala na wasambazaji nchini kote ili kuhakikisha wakulima wanapata bidhaa hizo kwa urahisi na kwa wakati.
Naye Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Innocent Keya, alisema uzinduzi wa viuatilifu hivyo ni hatua muhimu ya kuwakomboa wakulima wa Kanda ya Ziwa ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya wadudu wapya waharibifu wa mazao.
Alitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni uvamizi wa wadudu aina ya “Kantangaze”, ambao haukuwepo kwa kiwango kikubwa miaka iliyopita lakini sasa umeendelea kuathiri uzalishaji wa mazao katika baadhi ya maeneo.
“Upatikanaji wa viuatilifu vya kisasa utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kuwawezesha wakulima kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kutokana na mabadiliko ya mazingira,” alisema Keya.
Pia aliwataka mawakala wa pembejeo za kilimo kuhakikisha wanawapatia wakulima bidhaa zenye ubora na kuwapa elimu sahihi ya matumizi ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Balton Tanzania Ltd ni miongoni mwa kampuni zinazoongoza katika usambazaji wa viuatilifu na pembejeo za kilimo, ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 25 nchini Tanzania na katika mataifa mbalimbali barani Afrika. :::
Ends..

