ARUSHA MERU YAWEKEZA MAMILIONI KUBORESHA ELIMU YA KIMATAIFA ,MICHEZO NA UFADHILI WA VIPAJI, WANAFUNZI ZAIDI YA NCHI 15 DUNIANI WAHITIMU.
Na Joseph Ngilisho – Arusha
SHULE ya Kimataifa ya Arusha Meru iliyopo jijini Arusha, imeanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya miundombinu ya elimu na michezo, ikilenga kuboresha mazingira ya kujifunzia, kukuza vipaji vya wanafunzi na kuimarisha ubora wa elimu ya kimataifa, huku ikiendelea kutoa ufadhili wa masomo wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 120 kwa mwaka.
Akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa mwaka wa 6,11 na 13 wa mfumo wa Cambridge, uongozi wa shule hiyo ulieleza mikakati ya maendeleo inayolenga kuiweka Arusha Meru katika nafasi ya juu ya utoaji wa elimu bora nchini.
Mkurugenzi wa Bodi ya Shule hiyo ya kikataifa ya Arusha Meru , Jayesh Chandra, alisema skuli imejipanga kuimarisha ubora wa elimu kupitia ujenzi wa majengo mapya na kuboresha huduma muhimu kwa wanafunzi wa ngazi zote.
Alisema kwa sasa ujenzi wa jengo jipya la shule ya msingi unaendelea na unatarajiwa kukamilika kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo.
“Jengo hili litakuwa na maktaba ya kisasa kwa wanafunzi wa shule ya msingi pamoja na maabara ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT Lab) yenye kompyuta na vifaa vya kisasa ili kuwajengea msingi imara wa matumizi ya teknolojia tangu wakiwa wadogo,” alisema Chandra.
Aliongeza kuwa shule pia inajenga chumba maalumu cha sanaa na ubunifu (arts and crafts) pamoja na chumba cha michezo kitakachosaidia wanafunzi kujifunza nadharia na mbinu za michezo.
Kwa mujibu wake, mradi mkubwa zaidi ni ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo (Sports Arena) unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili.
“Uwanja huo utakuwa na taa za nishati ya jua, maeneo ya maegesho, njia bora za kupita na utaweza kutumika mchana na usiku. Lengo ni kuwapa wanafunzi nafasi ya kukuza vipaji vyao sambamba na masomo,” alisema.
Chandra alibainisha pia kuwa skuli inaendelea kuajiri walimu wa kimataifa kutoka Tanzania na nje ya nchi ili kuimarisha ubora wa elimu.
Alisema mwaka jana shule ilitoa ufadhili wa masomo wa zaidi ya Sh milioni 120, na mwaka huu imepanga kuzindua mpango mpya wa Talent Hunt Scholarship wenye thamani ya kati ya Sh milioni 120 hadi 150.
“Lengo letu ni kuwafikia watoto wenye vipaji lakini wasio na uwezo wa kifedha. Tunataka kujenga kizazi chenye maarifa na uwezo wa kushindana kimataifa,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa Arusha Meru ni taasisi isiyo ya kibiashara, hivyo mapato yote hurudishwa katika maendeleo ya shule.
Katika hatua ya kuwasaidia wazazi, alisema shule imeamua kutopandisha ada licha ya changamoto za kiuchumi.
“Tumebaki na viwango vilevile vya ada ili kuhakikisha elimu bora inaendelea kuwa nafuu kwa jamii,” alisema.
Mkuu wa Shule ya Arusha Meru International School, Mathews Silungwe, alisema shule itaendelea kutoa elimu ya kimataifa inayowajenga wanafunzi kitaaluma, kimaarifa na kifikra, hasa katika dunia ya sasa ya teknolojia na akili mnemba (AI).
Alisema mahafali hayo yamewakutanisha wahitimu wa mwaka wa 6,11 na 13 katika mfumo wa Cambridge, hatua muhimu katika safari yao ya elimu.
“Leo ni siku muhimu sana kwetu. Tumeshuhudia wanafunzi wakihitimu katika ngazi mbalimbali. Hii ni hatua kubwa na tunajivunia maendeleo yao kitaaluma na katika malezi ya tabia,” alisema Silungwe.
Alieleza kuwa mfumo wa Cambridge unawawezesha wanafunzi kujenga uwezo wa kufikiri kwa kina, kujieleza kwa kujiamini na kushindana kimataifa.
“Cambridge inamjenga mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuchambua, kuwasilisha mawazo yake na kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa na ya baadaye,” alisema.
Silungwe aliongeza kuwa dunia ya sasa inahitaji vijana wenye uelewa wa teknolojia na ubunifu, huku akibainisha kuwa AI ni sehemu muhimu ya mustakabali wa elimu na ajira.
“Tunakwenda katika dunia ya teknolojia. AI ipo kila mahali. Hii ni fursa kwa wanafunzi kujifunza na kukuza vipaji vyao,” alisema.
Pia alisisitiza kuwa shule hiyo inapokea wanafunzi kutoka mataifa na tamaduni mbalimbali bila ubaguzi.
“Shule ya kimataifa maana yake ni kutoa fursa sawa kwa kila mwanafunzi bila kujali anatoka wapi,” alieleza.
Silungwe aliwataka wahitimu kuiona safari ya kuhitimu kama mwanzo mpya wa maisha.
“Mahafali haya si mwisho wa masomo. Ni hatua ya kuingia ngazi nyingine. Elimu ni safari ya maisha yote,” alisema.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi, Priya Magesh, alisema mahafali hayo ni tukio muhimu katika kalenda ya shule na yalihudhuriwa na bodi ya shule, wazazi na wageni mbalimbali.
Alisema shule hiyo ya Cambridge inatumia mbinu shirikishi zinazowawezesha wanafunzi kufikiri, kuchambua na kutatua changamoto.
Kwa sasa kitengo cha msingi kina wanafunzi 445, huku shule ikiendelea kupanua miundombinu.
Alisema kuna ujenzi wa mabawa mapya ya madarasa, maabara mpya ya ICT, maktaba ya kisasa na uwanja mkubwa wa michezo kwa ajili ya kukuza vipaji.
“Tunajivunia mazingira bora ya kujifunzia yenye viwango vya kimataifa na usalama wa wanafunzi wetu,” alisema.
Magesh alitangaza kuwa mtihani wa Udhamini wa Vipaji (Talent Hunt Scholarship Examination) utafanyika Julai 4 katika viwanja vya shule.
Alisema mtihani huo uko wazi kwa wanafunzi wote na waliofanya vizuri watapata udhamini wa kupunguziwa ada.
“Tunawakaribisha wanafunzi wote kushiriki ili wapate fursa ya kusoma katika mazingira bora,” alisema.
Ends...




Post a Comment