POLISI MANYARA YAKUMBWA NA KASHFA NZITO ASKARI WAKE WAUA RAIA WASIO NA HATIA

 ASKARI WA POLISI MANYARA WAKUMBUKWA NA TUHUMA ZA MAUAJI YA RAIA, UCHUNGUZI WAANZA KWA KASI

Na Arushadigital, MANYARA

Jeshi la Polisi mkoani Manyara limejikuta katikati ya kashfa nzito kufuatia tuhuma zinazowakabili askari wake wawili wanaodaiwa kuhusika katika tukio la mauaji ya raia wasio na hatia, tukio lililozua taharuki na maswali mazito kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya dola.

Tukio hilo la kusikitisha liliripotiwa kutokea Aprili 22, 2026 katika Kijiji cha Minjingu, kilichopo Kata ya Nkaiti, Wilaya ya Babati, ambapo inadaiwa kuwa raia waliuawa katika mazingira yanayotia shaka huku tuhuma zikielekezwa kwa askari hao.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, tayari askari hao wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi pamoja na watu wengine wawili wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kubaini ukweli kamili wa kilichotokea.

“Uchunguzi unaendelea kwa umakini mkubwa ili kubaini mazingira halisi ya tukio hili. Hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika,” amesema Kamanda Makarani, akisisitiza dhamira ya jeshi hilo katika kusimamia haki.

Ameeleza kuwa ushahidi wa awali tayari umekusanywa na unatoa mwanga katika mwelekeo wa uchunguzi huo, huku jitihada zaidi zikifanyika kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika.

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo jamii imeonyesha wasiwasi mkubwa juu ya tukio hilo, ikitaka uwazi, haki na uwajibikaji kwa wahusika, hasa ikizingatiwa kuwa wanaotuhumiwa ni miongoni mwa wale waliokabidhiwa dhamana ya kulinda raia na mali zao.

Kamanda Makarani amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukamilisha uchunguzi huo kwa haraka, huku akiahidi kuwa Jeshi la Polisi halitafumbia macho vitendo vya ukiukwaji wa sheria hata vinapohusisha watumishi wake.

Wadau wa haki za binadamu na wananchi kwa ujumla sasa wanaelekeza macho yao katika mwenendo wa uchunguzi huo, wakisubiri kuona hatua madhubuti zitakazochukuliwa ili kuhakikisha haki inatendeka na imani ya wananchi kwa vyombo vya dola inaendelea kulindwa.

Ends..

Post a Comment

0 Comments