RC MAKALA AINGILIA MGOGORO WA MABILIONI KARATU, ATAKA HAKI NA UTULIVU KATIKA SEKTA YA UTALII
Na Joseph Ngilisho, KARATU
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Gabriel Makala, ameutolea kauli mgogoro mzito wa kifedha unaohusisha mwekezaji wa kigeni na mfanyabiashara mzawa katika Wilaya ya Karatu, akisisitiza umuhimu wa haki, uwazi na kulinda mazingira ya uwekezaji nchini.
Kauli hiyo ameitoa baada ya kukutana na pande zote mbili zinazohusika katika mgogoro huo, ambao unaihusu Kampuni ya uwekezaji ya Tarylin LTD inayomilikiwa kwa ubia na raia wa Uingereza, Timothy Flavell—mmiliki wa Manyara Safari Lodge—pamoja na Kampuni ya Travel Partner Limited inayomilikiwa na mzawa Erick Mashauri, ambaye alikuwa mpangaji wa jengo la biashara ya utalii.
ERICK MASHAURIChanzo cha mgogoro huo ni madai ya kifedha ambapo Timothy Flavell anamdai Mashauri kiasi cha dola za Marekani 26,000 akimtaka kulipa fedha hizo pamoja na kuondoka katika jengo hilo kufuatia kusitishwa kwa mkataba wake kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
Hata hivyo, upande wa Mashauri umekanusha vikali madai hayo, ukidai kuwa tayari ulitekeleza wajibu wake wa malipo kwa mujibu wa makubaliano ya awali, na kuibua tuhuma kuwa kuna njama za kutaka kumtapeli na kumwondoa katika biashara hiyo kwa njia zisizo halali.
Akizungumza baada ya kikao hicho, RC Makala amesema serikali haitavumilia migogoro inayoweza kuhatarisha taswira ya uwekezaji, hususan katika sekta nyeti ya utalii ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla.
“Ni lazima pande zote ziheshimu mikataba na sheria za nchi. Serikali ipo kuhakikisha haki inapatikana bila upendeleo, lakini pia inalinda wawekezaji na wazawa ili wote wanufaike na fursa zilizopo,” amesema Makala.
Ameongeza kuwa tayari ametoa maelekezo kwa vyombo husika kufuatilia kwa kina mkataba uliokuwepo kati ya pande hizo, ikiwemo kuchunguza uhalali wa madai ya kifedha na taratibu zilizotumika kusitisha mkataba huo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa suluhu ya amani na ya kisheria, akiwataka wahusika kuepuka kuchukua hatua zinazoweza kuongeza mvutano au kuathiri shughuli za utalii katika eneo hilo.
Wadau wa sekta ya utalii na uwekezaji wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mgogoro huo, wakieleza hofu kuwa unaweza kuathiri imani ya wawekezaji iwapo hautashughulikiwa kwa haki na uwazi.
Ends




0 Comments