NSSF YAAHIDI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA, YATOA VITANDA 80 NA MAGODORO 160 KWA SOBER HOUSES ARUSHA

NSSF YAAHIDI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA, YATOA VITANDA 80 NA MAGODORO 160 KWA SOBER HOUSES ARUSHA

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

KAIMU Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Arusha, Abubakar Soud, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kusaidia jamii, hususan makundi maalum yakiwemo waraibu wa dawa za kulevya wanaopatiwa huduma katika nyumba za upataji nafuu (Sober Houses).

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitanda 80 na magodoro 160 vilivyotolewa kwa nyumba hizo kwa kushirikiana na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Soud alisema msaada huo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na dawa za kulevya.

Alisema kupitia kauli mbiu ya NSSF inayosema “Tunajenga maisha yako ya sasa na baadaye,” mfuko huo umeona umuhimu wa kushiriki katika kusaidia waraibu kurejea katika maisha ya kawaida na kuwa sehemu yenye tija kwa jamii.

“Tumeguswa na kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika kuwahudumia waraibu. Hivyo, sisi pamoja na wenzetu wa PSSSF tumeamua kuunga mkono juhudi hizi kwa kutoa vitanda na magodoro kwa ajili ya nyumba za upataji nafuu,” alisema Soud.

Alieleza kuwa waraibu ni sehemu ya jamii na wengi wao ni wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, iwe katika sekta binafsi au serikalini, hivyo wanastahili kupata fursa na huduma zinazotolewa na mifuko hiyo.

Aidha, alisema NSSF inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, hususan kwa watu wa sekta binafsi na waliojiajiri, ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa.

“Mafao yetu yanajumuisha elimu, uzazi kwa kina mama, msaada wa mazishi, pensheni ya uzee, ulemavu pamoja na urithi. Tunatamani kuona hata waraibu wakijiunga na mifuko hii kwa sababu maisha ya baadaye yanahitaji maandalizi,” alisema.

Pia aliwahakikishia wananchi kuwa NSSF itaendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii ikiwemo ujenzi wa madarasa, utoaji wa madawati na misaada mingine yenye lengo la kuboresha ustawi wa wananchi.

“Milango yetu ipo wazi wakati wote kwa ajili ya kushirikiana na jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo,” alisisitiza.






Ends..

Post a Comment

0 Comments