By ArushaDigital | DODOMA
Mbunge Lukumay aibana TAMISEMI kuhusu changamoto za miundombinu Arumeru Magharibi
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Johannes Lembulung Lukumay, amekutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Riziki Silas Shemdoe, na kumweleza kwa uzito mkubwa changamoto zinazoikabili miundombinu ya barabara na madaraja katika jimbo hilo.
Katika mazungumzo hayo, Mbunge Lukumay ameeleza kuwa baadhi ya maeneo ya vijijini yamekuwa yakikabiliwa na changamoto kubwa za usafiri kutokana na ubovu wa barabara pamoja na kukosekana kwa madaraja imara, hali inayokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Changamoto zilizowasilishwa:
Ujenzi wa barabara ya Losinoni Juu – Kisimiri (km 12)
Ujenzi wa daraja la Mto Nduruma – Kata ya Nduruma
Ukarabati/ujenzi wa korongo la Enjikaka – Kata ya Oljoro
Mbunge huyo amesisitiza kuwa miradi hiyo ni muhimu kwa kuinua uchumi wa wananchi wa Arumeru Magharibi, hasa wakulima na wafanyabiashara wadogo wanaotegemea miundombinu hiyo kwa shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wake, Waziri Shemdoe alipokea maelezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa mujibu wa vipaumbele vya serikali katika kuboresha huduma za miundombinu nchini.




0 Comments