Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Awataka Maafisa Elimu Kuonesha Nidhamu na Uwajibikaji Kufanikisha Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini.
Na Joseph Ngilisho | Arusha
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, amewataka maafisa elimu wa mikoa na halmashauri kote nchini kuonesha nidhamu, uwajibikaji, na uthubutu katika usimamizi wa shule, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea jinsi rasilimali za elimu zinavyosimamiwa.
“Hakuna muda wa kuchelewesha masuala ya elimu. Kila afisa elimu lazima awe kielelezo cha nidhamu na uwajibikaji. Hatutavumilia udhaifu wowote katika usimamizi wa shule.
Watumishi wasiotimiza wajibu wao watachukuliwa hatua stahiki mara moja,” alisema Prof. Shemdoe wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania (REDEOA) jijini Arusha.
Waziri alibainisha kuwa miradi ya elimu inayotekelezwa bila nidhamu au uwajibikaji ni kupoteza rasilimali za taifa.
“Tunapaswa kuhakikisha kila mradi una thamani halisi ya muda na fedha, na kila mwanafunzi anapata elimu bora,” aliongeza, akisisitiza umuhimu wa data sahihi za wanafunzi, mpango wa chakula shuleni, na rasilimali za msingi ili kupunguza utoro na drop-out.
Aidha, Prof. Shemdoe aliwahimiza maafisa elimu kutumia mbinu za kisasa za uendeshaji wa shule, kuhakikisha ufuatiliaji wa maendeleo unakuwa wa karibu, na kuendeleza ushirikiano kati ya walimu, viongozi wa shule, na wadau wa elimu. “Leo, tuweke msimamo wa dhahiri: elimu ni kipaumbele, nidhamu ni wajibu, na maendeleo ya watoto wetu hayakubali ucheleweshaji!” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu), Atupele Mwambene, alithibitisha msisitizo huo kwa kupongeza jitihada za maafisa elimu na wadau. “Kila mchango wenu ni muhimu katika kuboresha ubora wa elimu.
Serikali inaweka mkazo mkubwa katika kutumia teknolojia na mbinu za kisasa kufanikisha utoaji wa elimu, kuhakikisha kila mwanafunzi anapata fursa sawa,” alisema Mwambene.
Mkutano wa REDEOA, uliohudhuriwa na maafisa elimu kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali, unalenga kubadilishana uzoefu, kuendeleza mbinu za kisasa za usimamizi wa shule, na kuimarisha maendeleo ya elimu.
Mwenyekiti wa REDEOA, Martin Nkwabi, alisisitiza kuwa mkutano huu ni fursa adhimu ya kuangalia changamoto, kuboresha mafunzo ya walimu, na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu yenye viwango vinavyokidhi malengo ya kitaifa.
Aidha, alibainisha kuwa uwekezaji wa serikali katika miundombinu ya shule, vifaa vya kufundishia, na malipo ya walimu umezaa matunda makubwa, ukipelekea ongezeko la ufaulu na ujio wa wanafunzi.
Wajumbe walipata nafasi ya kujadili mbinu za kisasa za uendeshaji wa shule, ufuatiliaji wa maendeleo, na kushughulikia changamoto za uhaba wa walimu na upatikanaji wa vifaa.
Naye Mwenyekiti wa CWT, Martin Nkwabi alisisitiza: “Mikutano kama hii ni msingi wa kuhakikisha Tanzania inafanikisha ndoto ya kuwa na mfumo wa elimu unaowezesha kila mtoto kufanikisha maendeleo yake ya kijamii na kiuchumi.”
ENDS ..




0 Comments