WANAFUNZI 15 CHUO CHA ARDHI TABORA MBARONI KWA KUMNG'OA MENO KWA KIPIGO MLINZI ,RC AAGIZA WATIMULIWE

 WANAFUNZI 15 CHUO CHA ARDHI TABORA WAKAMATWA KWA KUMSHAMBULIA MLINZI

RC Tabora aagiza wafukuzwe chuo mara moja

Na Joseph Ngilisho|TABORA


Wanafunzi zaidi ya 15 wa Chuo cha Ardhi Tabora, kilichopo Kata ya Cheyo katika Manispaa ya Tabora mkoani Tabora, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo wakituhumiwa kumshambulia mlinzi wa chuo hicho na kumsababishia majeraha, ikiwemo kumng’oa jino, baada ya kuzuka kwa mvutano uliotokana na tuhuma za kuzuiwa kuingia na kutoka chuoni muda wanaotaka.

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameagiza uongozi wa chuo hicho kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya wanafunzi waliobainika kuhusika na tukio hilo, ikiwemo kuwafukuza masomo mara moja kwa kuzingatia taratibu na kanuni za chuo.

Akizungumza chuoni hapo leo Machi 7, 2026, Chacha alisema taasisi za elimu haziwezi kuwa sehemu ya kulea au kuvumilia vitendo vya kihalifu, akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi muhimu katika kujenga mazingira bora ya kujifunzia.

“Nakupongeza mkuu wa chuo kwa hatua mlizochukua hadi sasa, lakini hakikisheni mnafuata sheria na taratibu za chuo kuwafukuza hawa watu. Hatuwezi kufuga wahalifu ndani ya taasisi za elimu,” amesema Chacha




Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora, Jeremiah Minja, ameeleza kuwa chanzo cha vurugu hizo kilianzia Machi 2, 2026, baada ya baadhi ya wanafunzi kwenda kuwahoji walinzi wa chuo wakidai kuna matukio ya kuibiwa nguo zao ndani ya mabweni.

Amesema walinzi hao walikanusha tuhuma hizo wakieleza kuwa jukumu lao ni kulinda usalama wa chuo, mali zake pamoja na wanafunzi, na si kuchukua mali binafsi za wanafunzi.

Minja amefafanua kuwa baadaye usiku wa siku hiyo majira ya saa mbili, baadhi ya wanafunzi walijaribu kupita katika eneo lisiloruhusiwa kama njia ya kutoka chuoni.

“Walipokamatwa na kuhojiwa na mlinzi aliyekuwa doria, walikataa kutoa ushirikiano. Badala yake walianza kupiga kelele na hatimaye kumshambulia mlinzi huyo kwa kumpiga na kumng’oa jino moja,” amesema Minja.

Ameongeza kuwa baada ya tukio hilo, uongozi wa chuo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ulifanikiwa kuwakamata wanafunzi wanaodaiwa kuhusika, huku uchunguzi ukiendelea kubaini washiriki wengine wa tukio hilo ili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria na kinidhamu.

Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu umuhimu wa nidhamu na uwajibikaji kwa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu, huku mamlaka zikisisitiza kuwa vitendo vya vurugu na uvunjifu wa sheria havitavumiliwa katika taasisi za elimu.

Ends

Post a Comment

0 Comments