JUMUIYA YA MADOLA YAIPOKEA DHAMIRA YA TANZANIA KURUHUSU UCHUNGUZI WA MASUALA YA DEMOKRASIA
Ujumbe Maalum ukiongozwa na Rais Mstaafu wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera, kutembelea Tanzania Machi 2026
Na Arusha Digital
Jumuiya ya Madola (Commonwealth) imeipokea na kuipongeza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuruhusu na kuwezesha ziara ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Dkt. Lazarus Chakwera, ambaye anatarajiwa kuongoza ujumbe maalum utakaofanya tathmini ya masuala ya demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu kufuatia matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hatua hiyo imeelezwa kufuatia kikao cha 72 cha Kamati Maalum ya Jumuiya ya Madola inayoshughulikia masuala ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu miongoni mwa nchi wanachama (CMAG), kilichofanyika Machi 7, 2026. Katika kikao hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Palamagamba Kabudi, alikutana na kamati hiyo na kufanya mazungumzo kuhusu maendeleo ya hali ya kisiasa na kidemokrasia nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na CMAG baada ya kikao hicho, kamati hiyo ilieleza kuridhishwa na hatua ya Tanzania kukubali kupokea na kushirikiana na ujumbe wa Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.
“CMAG pia ilikaribisha dhamira ya Tanzania ya kumpokea na kuwezesha ziara pamoja na kazi za Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu mwezi Machi 2026,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tanzania kwenye ajenda maalum ya CMAG
Hatua ya Tanzania kuendelea kujadiliwa katika vikao vya CMAG inatokana na maamuzi yaliyofikiwa katika kikao cha 71 cha kamati hiyo kilichofanyika Desemba 2025. Kikao hicho kiliongozwa na Dkt. Ian Borg, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Utalii wa Malta.
Katika mkutano huo, kamati iliamua kuiweka Tanzania kwenye ajenda maalum ya ufuatiliaji wa masuala ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu, ikiwa ni hatua ya kufuatilia utekelezaji wa masharti na mapendekezo yaliyotolewa kufuatia mjadala wa matukio yaliyoambatana na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
CMAG ilitoa masharti kadhaa kwa Tanzania, ikiwemo kuruhusu kikamilifu na bila vikwazo ziara ya ujumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, ili uweze kukutana na wadau mbalimbali wa kisiasa, kijamii na kiraia kwa uhuru na uwazi.
Aidha, Tanzania ilihimizwa kuhakikisha mazingira ya uhuru wa kukusanyika na kujieleza yanaheshimiwa, ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuathiri shughuli za vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari.
Mapendekezo ya mageuzi ya kisiasa
Mbali na hayo, kamati hiyo ilipendekeza kufanyika kwa jukwaa la mashauriano ya kisiasa litakalohusisha vyama vya siasa nchini, kwa lengo la kujenga mwafaka wa kitaifa kuhusu hatua za kuimarisha mfumo wa uchaguzi na mazingira ya kisiasa kuelekea chaguzi zijazo.
CMAG pia ilisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua za kisheria na kiutawala zilizo wazi dhidi ya wahusika wa vitendo vya vurugu vilivyoripotiwa wakati na baada ya uchaguzi, pamoja na kuhakikisha waathirika wa matukio hayo wanapatiwa haki zao, ikiwemo fidia pale inapostahili.
Ujumbe maalum kutembelea Tanzania
Ujumbe wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kuwasili nchini mwezi Machi mwaka huu utaongozwa na Rais Mstaafu wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera, ambaye ameteuliwa kuwa Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kufanya tathmini ya hali ya demokrasia, utawala wa sheria na utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na CMAG, pamoja na kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari.
Miongoni mwa nyaraka muhimu zitakazotumika kama rejea katika tathmini hiyo ni taarifa ya Tume Huru ya Uchunguzi kuhusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, tume ambayo iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua stahiki za kuchukuliwa.
Hatua ya kuruhusu ziara ya ujumbe huo inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Tanzania kuendelea kushirikiana na Jumuiya ya Madola katika kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na heshima kwa haki za binadamu miongoni mwa nchi wanachama.

0 Comments