VIONGOZI NGORONGORO WALAANI MAZAO YA WAKULIMA KUFYEKWA KWA AMRI YA DC ,MWENYEKITI WA HALMASHAURI ASEMA KITENDO HICHO HAKIKUBALIKI AAHIDI KUSHUGHULIKA NA JAMBO HILO BILA WOGA

 MWENYEKITI NGORONGORO AKERWA NA KUFYEKWA KWA MAZAO YA WANANCHI LOLIONDO, AAHIDI HATUA KALI

Na Joseph Ngilisho | NGORONGORO


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Manja Yaile, amekerwa na kitendo cha kufyeka mazao ya wakulima katika eneo la Loliondo One, akikitaja kuwa ni cha kinyume na taratibu na kinachowaumiza wananchi waliokuwa wakitegemea mazao hayo kwa maisha yao ya kila siku.

Tukio hilo limetokea katika Kata ya Orgosorock, Tarafa ya Loliondo, ambapo mazao ya mahindi ya wananchi yaliharibiwa katika mazingira yaliyozua taharuki na maswali mengi kuhusu uhalali wake pamoja na kukosekana kwa ushirikishwaji wa viongozi wa eneo husika.

Akizungumza na vyombo vya habari, Yaile amesema hatua hiyo imewaingiza hasara kubwa wananchi na kwamba haikuzingatia misingi ya sheria wala utawala bora.

“Hili ni jambo linalosikitisha sana.

Wananchi wamepata hasara kubwa, na sisi kama viongozi hatuwezi kulifumbia macho. Lazima hatua zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika,” alisisitiza Yaile

Amesema halmashauri haitavumilia maamuzi yanayofanywa bila kuzingatia sheria na maslahi ya wananchi, akiongeza kuwa uchunguzi wa kina utafanyika na hatua kali zitachukuliwa.

TUHUMA ZAMUELEKEA MKUU WA WILAYA

Taarifa za awali zinaeleza kuwa zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, jambo lililozua mjadala mkali miongoni mwa viongozi na wananchi.

Hata hivyo, juhudi za kumpata Sakulo kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi zimegonga mwamba, baada ya simu yake kuita bila kupokelewa kwa zaidi ya siku tano mfululizo. Chombo hiki kinaendelea kumtafuta.

CHANZO CHA MGOGORO

Eneo hilo linadaiwa kuwa chini ya usimamizi wa idara ya misitu ya halmashauri, ambapo mwaka 2025 wananchi walidaiwa kuvamia na kuanza kilimo. Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya aliwahi kuagiza kuwa kuanzia mwaka 2026 shughuli za kilimo zisitishwe.

Baadhi ya wananchi walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za uvamizi, lakini mwaka huu walishinda kesi baada ya mahakama kubaini hawana hatia.

Aidha, Februari mwaka huu, mbunge wa eneo hilo aliitisha mkutano wa hadhara na kufikia makubaliano kuwa wananchi waruhusiwe kuvuna mazao yao kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa, huku halmashauri ikipewa jukumu la kuweka mipaka rasmi.

Hata hivyo, hatua ya ghafla ya kufyeka mazao kabla ya kuvuna imeibua hasira na sintofahamu kubwa kwa wananchi.

VIONGOZI WA CHINI WALALAMIKA

Diwani wa Kata ya Orgosorock, Mohamed Bayo,(MAREKANI) amelaani kitendo hicho akisema kimekiuka misingi ya uongozi bora na ushirikishwaji wa wananchi.

“Ni jambo lisilokubalika kuona maamuzi makubwa kama haya yakifanywa bila kuwashirikisha viongozi wa eneo husika. Hii inaleta taharuki na kuondoa imani ya wananchi kwa serikali yao,” alisema Bayo.

Ameonya kuwa hatua kama hizo zinaweza kuchochea migogoro zaidi iwapo hazitashughulikiwa kwa kuzingatia sheria na hekima.

HALMASHAURI YASISITIZA HAKI ITENDEKE

Kwa upande wake, Mwenyekiti Yaile amesisitiza kuwa masuala ya ardhi na uhifadhi lazima yashughulikiwe kwa kufuata sheria na kulinda haki za wananchi.

Amesema halmashauri kwa kushirikiana na vyombo husika itaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu ili kuhakikisha wananchi walioathirika wanapata haki zao.

Mvutano huo sasa umeibua mjadala mpana Loliondo, huku wananchi wakisubiri hatua za mamlaka husika kurejesha haki na kumaliza mgogoro huo unaochukua sura mpya kila siku.





Ends..


Post a Comment

0 Comments