TRA ARUSHA YAKAZA USAJILI WASHAURI WA KODI, TATC YAFIKISHA WANACHAMA 268
Yasisitiza taaluma ni daraja muhimu kati ya walipa kodi na serikali
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha imeeleza dhamira yake ya kuendelea kusimamia kikamilifu usajili wa washauri wa kodi nchini, ikisisitiza kuwa taaluma hiyo ni kiungo muhimu kati ya walipa kodi na serikali katika kukuza mapato ya ndani.
Akifungua mkutano wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania (TATC) jijini Arusha, Meneja wa TRA Mkoa huo, Deogratius Shuma, alisema ni lazima wataalamu wote wa ushauri wa kodi kufuata taratibu za kisheria na kusajiliwa rasmi ili kulinda taaluma hiyo pamoja na maslahi ya walipa kodi.
Alifafanua kuwa washauri wa kodi wana nafasi kubwa katika kusaidia walipa kodi kuelewa sheria, kuandaa na kuwasilisha ritani, pamoja na kuhakikisha wanazingatia matakwa yote ya kikodi.
“Washauri wa kodi ni daraja muhimu sana kati ya TRA na walipa kodi. Wanasaidia kuongeza uelewa na kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari, jambo linalochangia ongezeko la mapato ya serikali,” alisema Shuma.
Aliongeza kuwa mchango wa wataalamu hao umeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kutokana na kuongezeka kwa uwajibikaji wa walipa kodi na uelewa wa sheria za kodi.
Katika kuendana na mabadiliko ya teknolojia, Shuma alisema TRA inaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali ikiwemo mfumo wa kisasa wa Integrated Domestic Revenue Administration System (IDRAS), ambao umerahisisha huduma mbalimbali kwa walipa kodi.
Kupitia mfumo huo, alieleza kuwa walipa kodi wanaweza kuwasilisha ritani, kuomba vyeti vya ulipaji kodi (tax clearance), kupata makadirio ya kodi pamoja na kushughulikia changamoto zao mtandaoni bila kulazimika kufika ofisini.
“Lengo letu ni kurahisisha huduma na kuongeza uwazi. Mlipa kodi anaweza kupata huduma zote akiwa mahali popote kupitia mfumo huu,” alisisitiza.
Aidha, alibainisha kuwa TRA imeanza kuunganisha mifumo yake na taasisi mbalimbali za serikali ili kuboresha upatikanaji wa taarifa, ambapo hadi sasa zaidi ya taasisi 15 zimeunganishwa, huku lengo likiwa kufikia taasisi zaidi ya 300.
Katika kulinda taaluma ya ushauri wa kodi, Shuma aliwataka wanachama wa TATC kushirikiana na TRA kuwabaini watu wanaofanya kazi hiyo bila usajili rasmi, akionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TATC, Sipieli Suka, alisema chama hicho kimeendelea kupiga hatua kwa kusajili wanachama 268 hadi sasa, hatua aliyosema inatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya chama hicho na TRA.
“Tumefanya kazi kwa karibu sana na TRA na mafanikio yanaonekana. Tumeweza kufikia wanachama 268 na tunaendelea kusajili wengine zaidi nchini kote,” alisema Suka.
Aliongeza kuwa chama hicho kimekuwa kikiendesha semina za kitaaluma kwa wanachama wake ili kuwajengea uwezo, kuongeza uelewa wa masuala ya kodi na kuimarisha weledi katika kazi zao.
“Semina hizi zinawasaidia wanachama wetu kubadilishana uzoefu na kukumbushana wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya taaluma,” alieleza.
Suka pia alisema TATC inaendelea kushirikiana na TRA kwa kutoa ushauri katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi na huduma kwa walipa kodi, jambo linalochangia kuongeza ufanisi wa sekta hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Mafunzo wa chama hicho, Sospeter Kibishi, alisema wataendelea kuimarisha mafunzo kwa wanachama ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sheria na taratibu za kodi.
Mkutano huo wa TATC umewakutanisha wataalamu wa kodi kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili changamoto, fursa na mikakati ya kuimarisha taaluma ya ushauri wa kodi Tanzania.
Ends..



0 Comments