DIRA YA MAENDELEO 2050 YALENGA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA UCHUMI NA TEKNOLOJIA
Waziri Mkuu awataka wadau kuandika historia ya mafanikio ya Taifa
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo inayotarajiwa kutumika hadi mwaka 2050 inalenga kuharakisha mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia, huku akiwataka wadau wa maendeleo na elimu kwa umma kushiriki kikamilifu kuandika na kusambaza historia ya mafanikio ya nchi.
Akizungumza leo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 110 wa Wadau wa Elimu kwa Umma, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa ni wakati muafaka kwa taifa kuangalia nyuma na kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha utekelezaji wa dira ya maendeleo iliyopita ya miaka 25, ili kujenga msingi imara wa dira mpya.
Alieleza kuwa katika kipindi hicho, Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali muhimu ikiwemo mawasiliano, miundombinu, afya pamoja na huduma za kijamii, hatua ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa.
“Ni muhimu kwa wadau wote, hususan wale wanaojihusisha na elimu kwa umma, kuhakikisha wanatengeneza vipindi, makala na maudhui yatakayowawezesha wananchi kuelewa safari ya maendeleo ya nchi yetu tangu tulipotoka hadi tulipofikia sasa,” alisema.
Dk. Nchemba alibainisha kuwa sekta ya mawasiliano ni miongoni mwa maeneo yaliyoonyesha mageuzi makubwa, akieleza kuwa hapo awali huduma hizo zilikuwa na changamoto nyingi ikiwemo upatikanaji mdogo na gharama kubwa, lakini sasa zimeimarika kwa kiwango kikubwa kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali katika miundombinu ya TEHAMA.
Aidha, alisisitiza kuwa dira mpya inalenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, sambamba na kuimarisha ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kukidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumzia mabadiliko ya kijamii na kiteknolojia, Waziri Mkuu alisema vijana wa kizazi cha sasa hawawezi tena kufahamu baadhi ya mifumo ya zamani kama matumizi ya stempu na masanduku ya posta, jambo linalodhihirisha namna ambavyo dunia imebadilika kwa kasi.
Kwa mujibu wake, hali hiyo inaweka wajibu mkubwa kwa wadau wa elimu na wachambuzi wa masuala ya umma kuhakikisha wanatunza kumbukumbu sahihi za maendeleo ya taifa ili vizazi vijavyo viweze kuelewa historia hiyo.
Katika sekta ya elimu, Dk. Nchemba alitoa mfano wa ongezeko kubwa la taasisi za mafunzo ya ufundi, akisema kuwa mara baada ya uhuru kulikuwa na shule tano tu za ufundi, zikiwemo Ifunda, Tanga na Moshi, lakini sasa zimeongezeka hadi kufikia 103.
Alieleza kuwa hatua hiyo imeongeza fursa kwa vijana kupata elimu ya ufundi na stadi za kazi, jambo linalochangia kupunguza ukosefu wa ajira na kuimarisha uchumi wa viwanda.
Kwa ujumla, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa mafanikio yaliyofikiwa ni msingi muhimu wa kuijenga Tanzania ya kisasa zaidi ifikapo mwaka 2050, huku akihimiza ushirikiano wa wadau wote katika kufanikisha utekelezaji wa dira hiyo mpya.
Ends..


0 Comments