LUKUVI AFARIKI DUNIA, TAIFA LAOMBOLEZA
By Arushadigital-DODOMA
Taifa limeingia kwenye maombolezo kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Isimani na aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, aliyefariki dunia leo Machi 25, 2026.
Taarifa za kifo hicho zimetangazwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye alieleza kuwa kiongozi huyo amefariki majira ya saa moja asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, marehemu Lukuvi alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la moyo, hali iliyosababisha kifo chake akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia alieleza masikitiko makubwa ya serikali na wananchi kwa kumpoteza kiongozi huyo aliyekuwa na mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo ya taifa. Alituma pole kwa Spika wa Bunge, familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Isimani pamoja na Watanzania wote kwa ujumla.
“Mhe. Lukuvi alikuwa kiongozi mwenye uzoefu, aliyejitolea kwa dhati kulitumikia taifa lake katika nyadhifa mbalimbali za uongozi. Tutaendelea kuukumbuka mchango wake,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Katika kipindi cha uhai wake, Lukuvi aliwahi kushika nafasi mbalimbali serikalini, akijizolea heshima kutokana na utendaji wake na msimamo wake katika kusimamia sera, uratibu wa shughuli za serikali pamoja na masuala ya watu wenye ulemavu.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa kisiasa na kijamii, hususan kwa wananchi wa Jimbo la Isimani ambao walimtegemea kama mwakilishi wao bungeni.
Mipango ya mazishi na taratibu nyingine za kitaifa zinatarajiwa kutangazwa na serikali kadri maandalizi yatakavyokamilika.
Taifa linaendelea kuomboleza kifo cha kiongozi huyu huku viongozi mbalimbali wa kisiasa na kijamii wakitarajiwa kuendelea kutoa salamu za pole na kumbukizi za mchango wake.
Ends..


0 Comments