SHEIKH HARUNA AHIMIZA DUA NA AMANI, TWARIQA KUENZI URITHI WA MTIMKAVU KWA KUFUTURISHA MAMIA ZAWIA KUU !

 SHEIKH HARUNA AHIMIZA DUA NA AMANI, TWARIQA KUENZI URITHI WA MTIMKAVU KWA KUFUTURISHA MAMIA

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA


Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya Dini ya Kiislamu ya Twariqa Tanzania, Sheikh Haruna Hussein, ametoa wito kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuendeleza dua, amani na mshikamano katika nusu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, akisisitiza kuwa kipindi hiki ni cha toba, kujisafisha na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo March 04,2026  Zawia Kuu jijini Arusha, Sheikh Haruna alisema Ramadhani ni zaidi ya kujizuia kula na kunywa, bali ni safari ya kurekebisha nafsi na kuimarisha maadili katika jamii.

“Tunapaswa kuitumia Ramadhani kama darasa la kujitathmini, kuimarisha udugu na kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie rehema na amani katika taifa letu,” alisema.


Katika maelezo yake, Sheikh Haruna alitangaza kuwa kesho Taasisi ya Twariqa itaandaa tukio kubwa la kufuturisha mamia ya Waislamu kutoka mikoa mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya kuenzi na kuendeleza urithi wa aliyekuwa kiongozi wao marehemu Salim Daruweshi maarufu kwa jina la Mtimkavu.

Alisema marehemu Mtimkavu alikuwa na utaratibu wa kufuturisha Waumini katikati ya mwezi wa Ramadhani kila mwaka, akilenga kuimarisha mshikamano na kusaidia wasiojiweza.

“Kesho tunakusanyika si kwa ajili ya iftar pekee, bali pia kumuombea dua kiongozi wetu aliyetuachia misingi ya upendo, umoja na kujali wengine. Tunaendeleza alichokianzisha,” alieleza.

Sheikh Haruna aliongeza kuwa tukio hilo litaambatana na dua maalum ya kuliombea taifa, viongozi wake na dunia kwa ujumla, hasa katika kipindi ambacho ulimwengu unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisisitiza kuwa amani ya nchi ni jukumu la kila mwananchi na kwamba Waumini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuilinda kwa njia ya maombi na matendo mema.

“Tunapoomba dua, tunaomba Mwenyezi Mungu atuepushe na migawanyiko, atujaalie hekima na kulinda umoja wetu. Ramadhani ni mwezi wa kurejesha matumaini,” alisema.

Alimaliza kwa kuwakaribisha Waislamu wote kushiriki tukio hilo kwa wingi, akisisitiza kuwa kuenzi urithi wa viongozi waliotangulia ni sehemu ya kuimarisha misingi ya kiroho na kijamii katika taifa.


Ends

Post a Comment

0 Comments