Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha limepitisha bajeti ya jumla ya shilingi bilioni 150 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha maendeleo ya miundombinu na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wa jiji hilo.
Bajeti hiyo ilipitishwa Machi 5, 2026 katika kikao rasmi cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jijini Arusha, ambapo madiwani walijadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi yatakayotekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa fedha kuanzia Julai 2026 hadi Juni 2027.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, kati ya fedha zote zilizoidhinishwa, kiasi cha shilingi bilioni 60.4 kinatarajiwa kukusanywa kupitia vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, ikiwemo ushuru wa huduma, tozo mbalimbali za halmashauri pamoja na mapato yatokanayo na shughuli za kiuchumi ndani ya jiji.
Sehemu kubwa ya bajeti hiyo imeelekezwa katika miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya mipangomiji na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mji pamoja na mahitaji ya wananchi.
Katika bajeti hiyo, zaidi ya shilingi bilioni saba zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya mipangomiji na uboreshaji wa miundombinu ya barabara za ndani ya jiji, hatua inayolenga kurahisisha usafiri wa wananchi, kupunguza msongamano wa magari na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Arusha.
Aidha, kiasi cha shilingi bilioni nne kimetengwa mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa barabara za vumbi pamoja na ujenzi na uboreshaji wa mitaro ya maji ya mvua, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza athari za mafuriko ambazo zimekuwa zikijitokeza katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo hasa wakati wa msimu wa mvua.
Katika mpango wa kuboresha miundombinu ya barabara za ndani ya jiji, halmashauri imepanga kujenga na kuboresha jumla ya kilomita 1.9 za barabara katika maeneo mbalimbali.
Sambamba na hilo, kutafanyika pia uwekaji wa kamera za usalama (CCTV) katika baadhi ya maeneo ya barabara ili kuongeza ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na kusaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu.
Vilevile, baraza hilo limeidhinisha mpango wa kuboresha jumla ya masoko 10 yaliyopo ndani ya Jiji la Arusha.
Hatua hiyo inalenga kuwapatia wafanyabiashara wadogo na wa kati mazingira bora na salama ya kufanyia biashara, sambamba na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.
Madiwani wameeleza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo ya jiji hilo kwa kuimarisha miundombinu, kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi
Halmashauri ya Jiji la Arusha imeeleza kuwa itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa bajeti hiyo ili kuhakikisha miradi iliyopangwa inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati, kwa lengo la kuinua ustawi wa wakazi wa jiji hilo pamoja na kuifanya Arusha kuendelea kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi na utalii nchini.
Ends...





0 Comments