RC MAKALA AFUATA NYAYO ZA WAZIRI MKUU MWIGULU,ATOA MAELEKEZO MAZITO KUSIKILIZWA KERO ZA WANANCHI ARUSHA

 RC Makalla Atoa Maelekezo Mazito Kusikiliza Kero za Wananchi Arusha

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA 


Mkuu wa Mkoa wa Arusha , Amos Makalla, ametoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi ya wilaya na halmashauri kuongeza kasi ya utatuzi wa kero za wananchi, akisisitiza uwajibikaji na ukaribu wa huduma kwa jamii.

Akizungumza Februari 27, 2026 katika kikao kazi kilichowakutanisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watumishi wa halmashauri za Meru , Arusha District na Arusha City, RC Makalla alisema migogoro ya ardhi imeendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.

Amesema ili kuharakisha upatikanaji wa haki na kupunguza malalamiko yasiyoisha, maafisa ardhi wa halmashauri wametakiwa kutenga siku ya Jumatano ya kila wiki kwa ajili ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya migogoro ya ardhi. Alisisitiza kuwa malalamiko yaliyo ndani ya uwezo wa mamlaka husika yashughulikiwe kwa haraka na kwa uwazi.

“Huduma za serikali zinapaswa kumfikia mwananchi kwa wakati. Kila kiongozi awajibike kwa nafasi yake ili kuondoa malalamiko yanayoweza kuzuilika,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, RC Makalla amewataka watendaji wa kata na vijiji nao kutenga siku ya Jumatano ya kila wiki kusikiliza kero za wananchi katika maeneo yao, huku wakurugenzi wa halmashauri wakitakiwa kuanzisha madawati maalum ya kushughulikia kero ndani ya ofisi zao.

Aidha, wakuu wa wilaya wameagizwa kutenga angalau siku moja kila mwezi kufanya ziara za kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja katika maeneo yao ya utawala, hatua inayolenga kuimarisha mawasiliano kati ya serikali na wananchi.

Mbali na usikilizaji wa kero, Mkuu wa Mkoa aliagiza kamati za halmashauri kufanya ziara za mara kwa mara kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha ubora, uwazi na thamani halisi ya fedha za umma inapatikana.

Maelekezo hayo yanatarajiwa kuongeza uwajibikaji wa viongozi wa ngazi za chini na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.






Ends

Post a Comment

0 Comments