MAMA MWENYE WATOTO WANNE APATA MSAADA WA MILIONI 1.8 BAADA YA KILIO CHAKE KUSIKIKA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MAMA mwenye watoto wanne, Flora Mbeve, amepokea msaada wa shilingi milioni 1.8 kwa ajili ya kulipa deni la vikoba lililokuwa likimkabili, baada ya kilio chake kusikilizwa na serikali.
Msaada huo umekabidhiwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, kufuatia agizo la Mwigulu Nchemba, baada ya kiongozi huyo kusikiliza kwa karibu changamoto za mama huyo katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Soko la Kilombero jijini Arusha.
Akizungumza kwa hisia baada ya kupokea msaada huo, Flora alisema alibaki na jukumu la kuwalea watoto wake peke yake baada ya kuachwa na mwanaume aliyekuwa akiishi naye kwa miaka 14, aliyedai kuwa sababu ya kuondoka ni kuzaliwa kwa watoto wa kike pekee.
“Niliachwa na mzigo wa malezi ya watoto pamoja na deni la vikoba la shilingi milioni 1.8. Hali hii ilininyima usingizi na kunifanya niishi katika mawazo makubwa ya namna ya kurejesha fedha za kikundi,” alisema.
Flora alieleza kuwa alijaribu kufuatilia haki za mtoto kupitia vyombo vya sheria, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda baada ya mzazi mwenzake kukataa kushirikiana katika mchakato wa kisheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha alisema msaada huo ni sehemu ya juhudi za serikali kusaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto nzito za kijamii na kiuchumi, hasa wanawake wanaobeba jukumu la malezi bila msaada.
Wanachama wa kikundi cha vikoba wanachotumia mama huyo walieleza kuwa walikuwa wakimtambua Flora kama mwanachama halali, hivyo walikuwa wakisisitiza urejeshwaji wa fedha ili kulinda mzunguko wa mfuko wa kikundi.
Flora alihitimisha kwa kuishukuru serikali kwa msaada huo akisema umeondoa mzigo mzito uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu na kumrejeshea matumaini ya maisha mapya pamoja na watoto wake.
“Ninafurahi sana. Fedha hizi zilikuwa zinaninyima usingizi. Leo najisikia huru na nina matumaini mapya,” alisema.
Ends







0 Comments