**JKCI YATUMIA ZAIDI YA SH BILIONI 1 KILA MWAKA KUSAIDIA WAGONJWA WASIO NA UWEZO
ZAIDI YA WANANCHI 1,000 WANUFAIKA HUDUMA ZA AFYA BURE ARUSHA**
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge amesema taasisi hiyo hutumia zaidi ya shilingi bilioni moja kwa mwaka, sawa na takribani shilingi milioni 200 kwa mwezi, kugharamia matibabu ya wagonjwa wa moyo wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu hayo, ambazo kwa kawaida ni kubwa kutokana na ubingwa na teknolojia inayohitajika.
Dkt. Kisenge ameyasema hayo leo January 03,2026 katika hospitali ya ALMC mkoani Arusha wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za upimaji na uchunguzi wa afya bure, ambapo zaidi ya wananchi 1,000 wa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani wamenufaika kupitia Mpango wa Tiba Mkoba wa Dkt. Samia Suluhu Hassan (Outreach Program).
Alisema mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha huduma za kibingwa za afya, hususan magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza, zinawafikia wananchi wengi zaidi bila kujali uwezo wao wa kifedha.
Huduma hizo zimetolewa na timu ya madaktari bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiongozwa na Dkt. Kisenge, bingwa wa magonjwa ya moyo, ambapo zoezi hilo limefanyika kwa kipindi cha siku kadhaa kuanzia tarehe 3 hadi 7 mkoani Arusha.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Dkt. Kisenge alisema lengo kuu la kambi hiyo ni kuwahamasisha wananchi kupima afya mapema ili kugundua magonjwa kabla hayajaleta madhara makubwa kiafya.
“Upimaji wa mapema humsaidia mtu kugundua tatizo kabla halijawa kubwa na kuepusha madhara makubwa kama kushindwa kwa moyo, figo au kupata kiharusi,” alisema Dkt. Kisenge.
Huduma zilizotolewa ni pamoja na vipimo vya moyo vya Echo na ECG, pamoja na vipimo vingine muhimu vya magonjwa yasiyoambukiza, vyote vikifanyika bila malipo yoyote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi kadhaa wamebainika kuwa na matatizo mbalimbali ya moyo, ambapo wagonjwa 36 wamepatiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu ya kibingwa zaidi.
Alisema baadhi ya wagonjwa hao wanahitaji kufanyiwa uchunguzi maalum wa mishipa ya damu ya moyo kwa kutumia mtambo wa Cath Lab, huku wengine wakihitaji kufanyiwa upasuaji wa kuziba matundu ya moyo au kuanzishiwa matibabu ya kudhibiti shinikizo la damu.
Aidha, wananchi waliogundulika kuwa na shinikizo la damu bila wao kufahamu wamepatiwa elimu ya lishe bora, ushauri wa kitaalamu pamoja na kuanzishiwa dawa, hatua inayolenga kuwakinga dhidi ya madhara makubwa ya baadaye ikiwemo figo kushindwa kufanya kazi na moyo kuchoka.
Dkt. Kisenge amewahimiza wananchi wa Jiji la Arusha na mikoa ya pembezoni katika Kanda ya Kaskazini kuendelea kujitokeza kupata huduma za uchunguzi wa afya mara kwa mara, akisisitiza kuwa mtu anaweza kuonekana mzima lakini akawa na tatizo kubwa la moyo linalohitaji matibabu ya haraka.
Katika hatua nyingine muhimu, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeingia makubaliano na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), ambapo hospitali hiyo itatoa huduma za magonjwa ya moyo chini ya usimamizi wa JKCI kwa kipindi cha miaka 20.
Kupitia ushirikiano huo, huduma za uchunguzi na matibabu ya awali ya magonjwa ya moyo zitapatikana Arusha, huku huduma zote za upasuaji wa kibingwa zikiendelea kufanyika chini ya usimamizi wa JKCI.
Uamuzi huo umetokana na umuhimu wa Mkoa wa Arusha kama kitovu cha utalii na maandalizi ya mashindano ya AFCON, hali itakayosaidia kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na wageni bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam.
Kwa sasa, wananchi wote wenye matatizo ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza wanahimizwa kufika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre, ambayo sasa inatoa huduma hizo chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
Ends..

0 Comments