MSIBA MZITO MUSOMA: MTUMISHI WA WIZARA YA MAJI, MKE NA MTOTO WAFARIKI KWA MOTO
Na ArushaDigital
Msiba mzito umeikumba Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara, baada ya familia ya watu watatu kufariki dunia kufuatia ajali ya moto ulioteketeza nyumba yao iliyopo Mtaa wa Nyarusrya. Waliopoteza maisha katika tukio hilo ni mtumishi wa Wizara ya Maji, Rochi Mkolekuwa (39), mke wake Mariam Msigwa (34) na mtoto wao Rochi Shaban (4).
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha, akieleza kuwa chanzo cha moto huo bado hakijabainika na kwamba uchunguzi wa kina umeanza mara moja kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama.
Kwa mujibu wa Kamanda Magere, Jeshi la Zimamoto lilipokea taarifa za ajali hiyo majira ya saa 10 usiku wa kuamkia leo, Jumatatu Januari 5, 2026. Hata hivyo, alipofika katika eneo la tukio, nyumba hiyo ilikuwa tayari imeteketea kabisa na wakazi wake wote walikuwa wamefariki dunia.
“Inaonekana taarifa ilichelewa kutolewa, hivyo tulipowasili eneo la tukio tulikuta tayari moto umemaliza kazi yake. Mwili wa baba ulikutwa sebuleni, huku miili ya mama na mtoto ikikutwa chumbani. Uchunguzi umeanza ili kubaini chanzo halisi cha moto huo,” amesema Kamanda Magere.
Tukio hilo limeacha simanzi kubwa kwa majirani, ndugu na jamaa, huku wakazi wa mtaa huo wakieleza masikitiko yao makubwa na kuwataka wananchi kuwa waangalifu zaidi na matumizi ya vifaa vya moto majumbani, pamoja na kutoa taarifa mapema pindi ajali kama hizo zinapotokea.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara limeendelea kutoa wito kwa wananchi kuzingatia tahadhari za usalama wa moto na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kwa wakati, ili kuzuia au kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza katika matukio ya dharura.

0 Comments