WAZIRI AMEIR ATOA MSIMAMO MKALI CHUO CHA NELSON MANDELA (NM-AIST)ASISITIZA NI NGUZO YA MAPINDUZI YA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UCHUMI WA KIDIJITALI TANZANIA

 WAZIRI ATOA MSIMAMO MKALI: NM-AIST NI NGUZO YA MAPINDUZI YA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UCHUMI WA KIDIJITALI TANZANIA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

Serikali imesisitiza kuwa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ni mhimili muhimu wa kujenga Taifa lenye vijana wabunifu, wataalamu mahiri na uchumi unaotegemea sayansi, teknolojia na ubunifu, huku ikitoa maagizo ya kuharakishwa kwa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa hosteli na kuimarishwa kwa programu za akili unde (AI).

Kauli hiyo nzito imetolewa Februari 05, 2026 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (Mb.), wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya NM-AIST iliyopo wilayani Arumeru, mkoani Arusha.

Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mheshimiwa Mwinyi Ally Mwinyi, menejimenti ya Taasisi, wataalamu wa sayansi, wanafunzi na wadau mbalimbali, Mhe. Ameir amesema Serikali imelenga kwa dhati kujenga kizazi cha vijana chenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa, sambamba na kusukuma mbele mageuzi ya kidijitali.

“Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuona Tanzania inakuwa Taifa lenye vijana wabunifu, wenye ujuzi wa sayansi na teknolojia unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa. NM-AIST ni chachu muhimu ya kufikia dira hiyo,” aliema  Ameir.

Naibu Waziri amesema uanzishwaji wa NM-AIST unaendana kikamilifu na Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan nguzo ya tatu inayolenga uwezo wa watu, jamii iliyoelimika na nguvu kazi yenye ujuzi na ari.

Ameeleza kuwa uwekezaji katika taasisi hiyo ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa maendeleo ya Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla, kwa kuwa inazalisha wataalamu wa sayansi, teknolojia na ubunifu wenye ushindani wa kimataifa.

Katika hatua nyingine, Ameir ameupongeza uongozi wa NM-AIST kwa kusimamia vyema mradi wa ujenzi wa hosteli maalum kwa wanafunzi wa kike wakiwemo wenye watoto na mahitaji maalum, akisema ni mfano bora wa ubunifu unaolenga usawa wa kijinsia katika elimu ya juu ya sayansi na teknolojia.

Hata hivyo, ametoa agizo la moja kwa moja kwa Menejimenti ya Taasisi na Fundi Mkuu wa mradi huo kuhakikisha asilimia 20 iliyosalia ya ujenzi inakamilika kwa wakati, ikitekelezwa kwa mfumo wa Force Account ili wanafunzi waanze kunufaika mapema.

“Asilimia 80 iliyofikiwa ni ushahidi wa uwajibikaji na uzalendo, lakini kasi iongezwe ili mradi ukamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane,” alisisitiza.

Akizungumzia mageuzi ya kidijitali, Naibu Waziri amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kutekeleza mpango maalum wa kuimarisha uwezo wa Taifa katika Sayansi ya Takwimu, Akili Unde na Sayansi Shirikishi (DS/AI+), kupitia Programu ya Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+).

Ameeleza kuwa NM-AIST imeteuliwa kuwa kituo cha kambi maalum ya maarifa (Bootcamp) kwa wanufaika wa programu hiyo, inayoratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Katika ziara hiyo,  Ameir alipata fursa ya kuzungumza na vijana 50 wanaojiandaa kwenda nje ya nchi kusoma shahada za kwanza katika masuala ya AI na takwimu, akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa Taifa na kuzingatia maadili ya Kitanzania.

“Taifa linawategemea ninyi katika safari ya mageuzi ya kidijitali. Popote mtakapokuwa kumbukeni nyinyi ni Watanzania,” amesema.

Kabla ya kuhitimisha hotuba yake, Naibu Waziri ametoa maelekezo kadhaa yakiwemo:

NM-AIST kusaidia wanafunzi wa Bootcamp kuomba ufadhili katika vyuo vikuu bora duniani ili kupunguza mzigo wa Serikali.

Taasisi kuendelea kujijengea hadhi ya kituo cha umahiri wa kikanda na kimataifa katika teknolojia zinazochipukia.

Menejimenti kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kupitia wadau wa maendeleo, sekta binafsi na miradi ya kimataifa ya utafiti.

Amehitimisha kwa kuwapongeza watumishi na wanafunzi wa NM-AIST kwa kuendeleza maono ya Hayati Nelson Mandela, akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii, nidhamu, ubunifu na uzalendo kwa manufaa ya Taifa.


Ends..

Post a Comment

0 Comments