DC MKUDE AZINDUA RASMI KAMPENI YA UHAMASISHAJI BIMA YA AFYA KWA WOTE ARUSHA

 DC MKUDE AZINDUA RASMI KAMPENI YA UHAMASISHAJI BIMA YA AFYA KWA WOTE ARUSHA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amezindua rasmi kampeni ya uhamasishaji wananchi kujiunga na Mpango wa Serikali wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua inayolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kwa uhakika bila vikwazo vya kifedha.

Uzinduzi huo uliofanyika leo Desemba 29, 2025 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuimarishwa kwa mfumo wa bima ya afya kwa wote ili kupunguza gharama za matibabu na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,  Mkude amesisitiza kuwa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni nguzo muhimu katika mageuzi ya sekta ya afya, na kuwataka watendaji wa serikali, madiwani pamoja na viongozi wa ngazi za mitaa kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kujiunga na mpango huo.

“Serikali imeamua kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya kwa uhakika. Bima ya Afya kwa Wote si anasa bali ni hitaji la msingi. Nawaagiza madiwani, watendaji wa mitaa na mabalozi kuwahamasisha wananchi wajiunge na mpango huu unaogharimu shilingi 150,000 tu kwa kila kaya,” alisema Mkude.

Aidha, aliwaelekeza wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya wilayani humo kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia miongozo, taratibu na kanuni zote zilizowekwa na Serikali, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Miraji Kisile-Ofisa NHIF ARUSHA

Kwa upande wake, Afisa Uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Arusha, Miraji Kisile, alisema mpango wa Bima ya Afya kwa Wote umejikita katika kuhakikisha wananchi wote wanajiunga kwa lazima ili kupata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha katika vituo vyote vinavyotoa huduma za afya nchini.

Alieleza kuwa mpango huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi mapema Januari 2026 na Rais Samia Suluhu Hassan, na utampa mwananchi au kaya iliyojiunga uhakika wa kupata matibabu popote nchini kupitia mfumo wa uchangiaji wa pamoja.

“Bima ya Afya kwa Wote si hiari bali ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wananchi wote, wakiwemo walio nje ya mfumo rasmi wa ajira, watumishi wa umma, wajasiriamali, wazee na makundi mengine,” alisema Kisile.

Alifafanua kuwa gharama ya uchangiaji ni shilingi 150,000 kwa kila kaya kwa mwaka, ikihusisha baba, mama na wategemezi wanne walio chini ya umri wa miaka 21. Mpango huo, alisema, utaondoa mzigo wa gharama kubwa za matibabu ambazo wananchi walikuwa wakizibeba hapo awali.

Kwa mujibu wa NHIF, mchango huo utawawezesha wanachama kupata huduma mbalimbali ikiwemo kumuona daktari, kufanya vipimo, kulazwa, kufanyiwa upasuaji mdogo na mkubwa pamoja na kupata dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za Serikali, pamoja na vituo vya dini na binafsi vitakavyoingia makubaliano na Serikali.

Kisile aliongeza kuwa zoezi la uandikishaji linatarajiwa kuanza mapema Januari 2026 kupitia ofisi za NHIF katika ngazi ya wilaya, kata na mitaa ili kuwafikia wananchi kwa urahisi.

Willfred Soilei-Mwkiti ccm(w)Arusha

Julias Sekeyani -Naibu Meya Arusha

Naye Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Julius Sekeyani, pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Wilfred Soilei, waliwataka madiwani na viongozi wote wa ngazi ya kata na mitaa kuunga mkono kikamilifu zoezi hilo kwa kuwahamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mara tu utakapozinduliwa rasmi na Rais Samia mapema mwakani.

Kwa ujumla, uzinduzi wa kampeni ya Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, kuboresha ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo ya sekta ya afya katika Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla, sambamba na dira ya Serikali ya kuhakikisha afya njema kwa kila Mtanzania.






Ends..

Post a Comment

0 Comments