Kanuni ya maudhui ya mtandao zamekiuka haki za binaadamu,zapingwa
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
MAHAKAMA ya Afrika ya Mashariki,leo Novemba 13, 2025, imesikiliza shauri linalopinga baadhi ya vifungu vya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA), likidai kwamba vinakiuka misingi ya haki za binadamu na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).
Shauri hilo namba 30/2020 limefunguliwa na mashirika manne ya utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania — Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), na Center for Strategic Litigation (CSL) — dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya majaji watano wa Mahakama hiyo: Jaji Johanes Masara, Jaji Richard Wejuri, Jaji Richard Muhumuza, Jaji Dkt. Gacuko Leonard na Jaji Kayembe Kasanda.
Mashirika Yadai Sheria Inaminya Uhuru wa Mawasiliano
Wakili Jeremiah Mtobesya na Peter Majanjala, waliowakilisha waleta maombi, waliieleza mahakama kwamba baadhi ya vifungu vya Kanuni za Maudhui Mtandaoni — ikiwemo vifungu 3, 4, 5, na 6 — vina mapungufu makubwa vinavyoweza kutumika kudhibiti uhuru wa kujieleza na kutoa taarifa.
> “Sheria yoyote inapaswa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, ikiwemo uhuru wa kupokea na kutoa taarifa. Lakini hata baada ya marekebisho ya mwaka 2022 na 2025, bado kuna vifungu vinavyokinzana na haki hizo za msingi,” alisema Mtobesya.
Aliongeza kuwa adhabu zilizowekwa, ikiwemo faini ya hadi Sh milioni 5 au kifungo cha miezi 12, ni kali kupita kiasi na zinaweza kuwatisha wananchi kutumia haki yao ya kujieleza mtandaoni.
Kwa upande wake, Wakili Majanjala alisema taratibu za utoaji leseni za maudhui mtandaoni ni tata na zisizo rafiki kwa watumiaji wote, kwani si kila anayetoa maudhui anafanya biashara.
> “Kanuni hizi pia zinakiuka vifungu vya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, hususan vifungu vya 6(d), 7 na 8(c), vinavyoelekeza nchi wanachama kuzingatia demokrasia, uwazi, utawala bora na haki za binadamu,” alieleza.
Ameomba mahakama itamke wazi kuwa vifungu hivyo vinapingana na Katiba ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na misingi ya haki za binadamu, hasa haki ya kujieleza na kupata taarifa.
Upande wa Serikali, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Stanley Kalokola akisaidiana na Daniel Nyakika, ulijibu hoja hizo kwa kueleza kuwa marekebisho yaliyofanyika tayari yameondoa mapungufu mengi yaliyokuwa yakilalamikiwa.
> “Kanuni za Maudhui hazikiuki haki za binadamu. Zinatoa mwongozo wa matumizi salama ya mtandao na kulinda maslahi ya taifa bila kuvunja haki za msingi,” alisema Kalokola.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Johanes Masara aliahirisha kesi hiyo na kusema tarehe ya hukumu itatangazwa baadaye.
Shauri hilo linatarajiwa kuweka historia muhimu kuhusu mipaka kati ya udhibiti wa serikali mtandaoni na uhuru wa mawasiliano katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Mwisho


0 Comments