NYAHIRI SEKONDARI ARUSHA, YAANZA KUTOA SCHOLARSHIP WANAFUNZI KADHAA WANUFAIKA NJE YA NCHI MKURUGENZI AHIMIZA UBUNIFU NA NIDHAMU AJIVUNIA UMAHILI

NYAHIRI SEKONDARI ARUSHA, YAANZA KUTOA SCHOLARSHIP WANAFUNZI KADHAA WANUFAIKA  NJE YA NCHI MKURUGENZI AHIMIZA UBUNIFU NA NIDHAMU AJIVUNIA UMAHILI

Na Joseph Ngilisho, Arusha


SHULE ya Sekondari Nyahiri iliyopo Kata ya Terat, Jijini Arusha, imefanya mahafali ya pamoja ya wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne kwa mbwembwe, shangwe na hamasa kubwa, huku mgeni rasmi akiwa ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Michael Kimbaki, ambaye aliwahimiza wahitimu kuthamini elimu, nidhamu na ubunifu kama nguzo muhimu za mafanikio katika maisha.


Akizungumza katika hafla hiyo leo Oktoba 4,2025  iliyohudhuriwa na wazazi, walimu, wanafunzi na wadau wa elimu, Kimbaki alisema shule ya Nyahiri imejipambanua kama taasisi kinara katika utoaji wa elimu bora yenye matokeo chanya, na imekuwa ikiandaa wanafunzi wenye nidhamu, ujasiri na uwezo wa kujitegemea.

> “Tumejenga mfumo wa kuwafanya wanafunzi wetu wawe wabunifu, wachapakazi na wanaojiamini. Tunawafundisha kutokuwa watu wa kukopi na kupesti, bali wafikiri na kubuni majibu yao kwa uelewa mpana,” alisema Kimbaki.

Aidha, Mkurugenzi Kimbaki alifichua kuwa shule hiyo imeanzisha mpango maalumu wa kuwatafutia ufadhili wa masomo nje ya nchi (Scholarship) kwa wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi katika masomo yao, kama njia ya kuwahamasisha kujituma zaidi.

> “Baada ya kubaini changamoto ya ajira na ushindani mkubwa katika soko la dunia, tumeanzisha programu maalumu ya kuwatafutia scholarship wanafunzi wetu wanaong’ara. Hadi sasa, wanafunzi watatu wamenufaika na ufadhili huo na wanasoma katika nchi za China, Uingereza na Uturuki,” alisema kwa fahari.


Katika hatua nyingine, Kimbaki alitangaza mipango kabambe ya maendeleo kwa shule hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala la kisasa lenye ukumbi wa mikutano, pamoja na bwalo la chakula na maktaba ya kisasa itakayowezesha wanafunzi kujisomea kwa ufanisi zaidi.

> “Tunataka Nyahiri iwe mfano wa shule bora za Arusha na Tanzania kwa ujumla. Tunajenga miundombinu ya kisasa itakayowasaidia watoto wetu kusoma katika mazingira mazuri, yenye hamasa ya ubunifu na utafiti,” aliongeza.


Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyahiri, Petro Mwita, aliwapongeza wahitimu kwa bidii na nidhamu waliyoionyesha kipindi chote cha masomo yao, huku akitoa shukrani kwa wazazi na walimu wote waliotoa ushirikiano mkubwa hadi kufanikisha safari ya elimu kwa vijana hao.

> “Tunajivunia kuona wanafunzi wetu wakifikia hatua hii muhimu. Safari ya elimu si rahisi, inahitaji kujituma na kujitambua. Nyahiri imekuwa kitovu cha malezi bora ya kielimu na kimaadili. Tunaamini kila mhitimu ataenda kuwa balozi mwema wa shule yetu,” alisema Mwalimu Mwita.


Aidha, aliwahimiza wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya heshima, bidii na upendo wa kujifunza.

> “Elimu ni urithi wa kudumu. Wazazi msichoke kuwekeza katika elimu ya watoto wenu; ndiyo njia pekee ya kuwafungulia milango ya mafanikio,” aliongeza.


Hafla hiyo ilinogeshwa na burudani mbalimbali ikiwemo nyimbo, michezo ya jukwaani na maonesho ya vipaji kutoka kwa wanafunzi, kuashiria furaha ya mafanikio. Wazazi na wageni waalikwa walionekana wakifurahia mafanikio ya shule hiyo ambayo imekuwa ikionyesha maendeleo ya haraka katika ubora wa elimu.

  






-ends..

Post a Comment

0 Comments