Mauaji ya Kikatili ya Mwanafunzi IFM: Polisi Wakaza Mnyororo, Wanne Watiwa Mbaroni
By Arushadigutal| Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa wanne kuhusiana na tukio la kinyama la mauaji ya James Rogers Temba, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM).
Mwili wa marehemu uligunduliwa Aprili 30, 2026 ukielea katika maji ya Mto Msimbazi, eneo la Kipawa, wilayani Ilala, ukiwa hauna kichwa—hali iliyozua hofu na maswali mengi miongoni mwa wakazi wa jiji hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, watuhumiwa waliokamatwa ni Steven Rogers Chaka (31), Anna Frank Lema (30), Twalibu Khamis (23) na Michael John (26), wote wakazi wa Dar es Salaam. Kukamatwa kwao kunatajwa kuwa sehemu ya operesheni maalum ya upelelezi iliyofanyika kwa umakini kufuatia tukio hilo lililogusa hisia za wengi.
Chanzo cha taarifa kutoka ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama kimeeleza kuwa uchunguzi wa awali unaendelea kuchunguza chanzo halisi cha tukio hilo, ikiwemo kubaini iwapo mauaji hayo yanahusishwa na migogoro binafsi, uhalifu wa kupanga, au sababu nyinginezo.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao pamoja na kukusanya ushahidi wa kisayansi ili kuhakikisha ukweli wa tukio unafahamika na haki inatendeka.
Aidha, Polisi wamewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kufanikisha uchunguzi huo, huku wakisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuhusika na tukio hilo.
Tukio hilo limeibua taharuki kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, hususan wanafunzi na jamii ya elimu, wakitaka mamlaka husika kuhakikisha usalama unaimarishwa na wahusika wote wanachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

0 Comments