By arushadigtal
TAKRIBAN watu 37 wamefariki na wengine kadhaa bado hawajulikani walipo baada ya boti ya watalii kupinduka nchini Vietnam wakati wa hali mbaya ya hewa.
Kisa hicho kilitokea katika Ghuba ya Ha Long, eneo maarufu la watalii kaskazini mwa nchi.
Abiria wengi waliripotiwa kuwa familia za Kivietinamu zinazozuru kutoka mji mkuu Hanoi.
Mvua kubwa imekuwa ikizuia shughuli ya kuwatafuta manusura, waokoaji wanasema, lakini kufikia sasa watu 11 wametolewa kwenye maji wakiwa hai.
Meli hiyo iliyopewa jina la Wonder Seas, ilikuwa imebeba watu 53 ilipopinduka baada ya kukumbwa na dhoruba ya ghafla, taarifa kutoka kwa Walinzi wa Mpaka wa Vietnam na jeshi la wanamaji ilisema.
Shahidi aliyejionea aliliambia shirika la habari la AFP kwamba anga ilikuwa giza mwendo wa 14:00 saa za huko Jumamosi (07:00 GMT).
Kulikuwa na "dhoruba ya mawe makubwa kama vidole vya miguu na mvua kubwa, radi na umeme", amesema.
Chanzo: BBC
0 Comments