KIJANA WA HOVYO AMUUA BABA YAKE NA KUMTUMBUKIZA KWENYE SHIMO LA CHOO

By arushadigtal


 Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linamshikilia Rajabu Hamis (23), mkazi wa Mtaa wa Muheza, wilaya ya Kibaha, kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Hamis Musa (50), katika tukio la kikatili lililotokea usiku wa Julai 11, 2025.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 18, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alimshambulia marehemu kwa kumpiga ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake, kabla ya kumburuza na kumtumbukiza kwenye shimo la choo.


“Wakati tukio hilo linatokea, majirani walikuwa wakisikia purukushani usiku huo. Asubuhi walipoamka waliamua kufuatilia na kugundua michirizi ya damu na miburuzo iliyoishia chooni, ndipo walipochukua hatua ya haraka kufanya jitihada za kumuokoa,” amesema Kamanda Morcase.



Baada ya kuokolewa kutoka kwenye shimo hilo, Hamis Musa alikimbizwa katika kituo cha afya kwa ajili ya matibabu, lakini kutokana na hali yake kuwa mbaya, alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tumbi, na hatimaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila.


Hata hivyo, juhudi za madaktari hazikuweza kuokoa maisha yake, ambapo Kamanda Morcase amethibitisha kuwa marehemu alifariki dunia alfajiri ya Julai 16, 2025, akiwa anaendelea na matibabu hospitalini hapo. Mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.


Akizungumzia chanzo cha tukio hilo la kusikitisha, Kamanda Morcase amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda sababu kuu ilikuwa ni mgogoro wa mali, hasa kuhusu umiliki wa nyumba. Hata hivyo, uchunguzi wa kina unaendelea na mara utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.



Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia kudhibiti vitendo vya ukatili na uhalifu katika jamii.

Post a Comment

0 Comments