Na Joseph Ngilisho Arusha
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti uchakachuaji wa mafuta kutoka asilimia 70 hadi chini ya asilimia 2 uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu na hivyo kufanya kiwango cha mafuta yanayoingia na kuuzwa nchini kuwa bora zaidi.
Aidha mamlaka hiyo imedhibiti ufumuko wa bei baada ya kuweka utaratibu wa bei elekezi jambo ambalo limesaidia bei ya bidhaa hiyo kutopanda kiholela na kuwapa unafuu wananchi.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa EWURA kanda ya kaskazini mhandisi Lorivii Long'idu wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake katika wiki ya huduma kwa wateja na kusisitiza kuwa lengo la EWURA ni kuhudumia wateja kwa viwango bora vinavyokubalika kimataifa .
Alisema kuwa EWURA imepiga hatua kubwa katika kusimamia ubora wa mafuta na kudhibiti uchakachiaji ikiwemo faini kubwa zinazotozwa na mamlaka hiyo kwa wafanyabiashara wachache wanaobainika kufanya uchakachuaji wa mafuta.
"EWURA tunajukumu la kuhudumia wateja kwa viwango vya kimataifa na kufikia malengo tuliyojiwekea ikiwemo utoaji wa leseni"
Alisema EWURA imejipanga vyema kudhibiti uchakachuaji wa mafuta hapa nchini ambapo awali ulifikia hadi asilimia 70 ,lakini kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kufikia chini ya asilimia 2
Alisema chamoto iliyopo kwa sasa ni baadhi ya maeneo ya pembezoni bado kuna wimbi la uingizaji wa mafuta ya magendo na hivyo uchakachuaji bado unafanyika lakini kwa kiwango kidogo sana na EWURA inaendelea kufuatilia.
Wakati huo huo amesisitiza kwa wafanyabiashara wa visima vya mafuta nchini ,kuhakikisha wanaingia mkataba na waagizaji wakubwa wa mafuta kutoka nje ya nchi wawe na mikataba ili kuwa na uhakika wa kupata bidhaa ya mafuta.
Kwa upande wake mfanyabiashara na mmiliki wa kituo cha mafuta cha Five star,Aliraza Gulam husein aliipongeza EWURA kwa huduma nzuri kwa wafanyabiashara wa mafuta .
Aliraza ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wauzaji wa mafuta mkoa wa Arusha (Tapsoa)ameiomba EWURA kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara hao kuhakikisha wanapata huduma ya uhakika ya mafuta kutoka kwa wauzaji wakubwa.
Aidha aliitaka EWURA kusimamia Vema ili kusaidia upatikanaji wa mafuta hapa nchini na kuondoa changamoto inayojitokeza na kusababisha uhaba wa mafuta nchini.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi EWURA kanda ya kaskazini,Muhiba Chakupewa alisema moja ya mafanikio ya mamlaka hiyo ni pamoja na kupunguza uchakachuaji wa mafuta kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na hapo awali ambapo kulikua na changamoto kubwa.
" Tumefanikiwa kudhibiti uchakachuaji wa mafuta
na wale waliokuwa wakijihusisha wanakutana na faini kubwa "
Alisema mafanikio mengine kwa wateja ni kuhakikisha wafanyabiashara wa nishati na maji wanakuwa na leseni na kutatua malalamiko yao.
Ends..
0 Comments