Na Joseph Ngilisho ARUMERU
Wazazi wametakiwa kuongeza uangalizi kwa watoto wao wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari kufuatia uwepo wa vitendo vya ubakaji na ulawiti vilivyoshamiri hapa nchini ikiwemo wilaya ya Arumeru,mkoa wa Arusha.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya hiyo,Emanuela Kaganda wakati alipokuwa kwenye mahafali ya 15 ya wahitimu 188 wa darasa la saba na sekondari katika shule zenye mchepuo wa kiingereza za Newlife chini ya shirika la Newlife outreach,zilizopo Olosiva wilayani humo na sokoni 1 jijini Arusha .
Alisema hivi sasa wimbi la ubakaji na ulawiti limekuwa kubwa na hivyo aliwataka wazazi kuwalinda watoto wao hasa kipindi hiki wakisubiri matokeo yao ya mtihani wakiwa nyumbani baada ya kuhitimu masomo yao .
"Tunaomba sana wazazi mkatenge muda wa kuendeleza malezi bora kwa watoto wenu mkaangalie mienendo yao na kuendelea kuwapa miongozo wakati wanasubiri kuendelea na masomo mengine tunapenda kuona ndoto zao zikitimia"
"Ndugu zangu mimi ni mkuu wenu wa wilaya ya Arumeru maadili sasa yamebadilika ukienda kwenye kituo chetu cha polisi Usariver ukikuta wahalifu kumi wapo mahabusu ,ujue nane wanamakosa ya ubakaji au ulawiti"
Aidha Kaganda alipongeza Newlife outreach kwa kuhakikisha inaunga mkono jitihada za serikali katika uwekezaji wa elimu ili kuwapatia watoto elimu iliyo bora na kuwataka wahitimu kuzingatia malezi bora waliyoyapata shuleni.
Awali mwanzilishi wa shirika la Newlife outreach,dkt Egon Falk alisema ndoto yake ni kuona watoto wa jamii ya kitanzania wanapa elimu bora na pia wanapata malezi ya kiroho ili kujiepusha na matukio yasiyo mpendeza mungu
Dkt Egon ambaye ameishi hapa nchini kwa miaka 49 kama m-missionary akitokea nchini Denmark ,alisema anatamani kuona elimu wanayoipata inawasaidia na hata kufikia kuwa viongozi wakubwa na hata rais wa nchi anapatikana kutoka kwa wahitimu wa shule hiyo kwa sababu wamelelewa katika maadili mema.
"Niwaombe Radhi wanawake wote, zamani sisi wazungu tuliamini kuwa wanawake hawana uwezo wa kuongoza lakini kwa sasa nimeshuhudia akina mama wanachukua madaraka makubwa na wanafanya vizuri, nimpongeze sana rais wetu Samia Suluhu Hassan "
Naye meneja wa shule za Newlife ,Nicolas Sawa alisema kuwa jumla ya wahitimu wapatao 188 wamemaliza masomo yao katika shule tatu wakiwemo wahitimu 57 wa kidato cha nne ,wahitimu 82 wa darasa la saba na wahitimu 59 wa darasa la awali(chekechea).
Alisema shule hiyo imekuwa na utaratibu wa kuchukua watoto wenye uwezo mdogo wa kielimu ili kuwapatia elimu bora na kufikia uwezo mzuri wa kimasomo.
Alisema lengo la shirika la Newlife outreach ni kuwekeza kwenye elimu itakayowasaidia watoto kuwatoa kwenye utumwa ili mwanafunzi aweze kujitegemea.
Naye katibu wa ccm mkoa wa Arusha,Musa Matoroka alilipongeza shirika la Newlife outreach kwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu ,ikiwa ni mapokeo chanya ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kutekeleza ilani ya ccm kuhakikisha watoto wanapata elimu bora hapa nchini.
"Nazipongeza shule zote za Newlife kupitia shirika lake la Newlife outreach kwa matokeo mazuri ya mtihani kwa wanafunzi kufaulu vizuri naimani mnatekeleza vema ilani ya ccm kupitia jitihada za serikali za kutaka kila mtoto apate elimu bora"
....Ends...
0 Comments