SUPERDOLL YALENGA SOKO LA MIGODI KWA MATAIRI YA MITAMBO MIKUBWA
..Yavutia wachimbaji na wawekezaji maonesho ya madini, yaeleza upanuzi wa huduma mikoani
Na Joseph Ngilisho | DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Superdoll imejipanga kuongeza wigo wa biashara katika sekta ya madini nchini kupitia usambazaji wa matairi ya mitambo mikubwa ya uchimbaji pamoja na vipuri mbalimbali vinavyotumika katika shughuli za migodi.
Kampuni hiyo imesema maonesho ya madini na uwekezaji yanayofanyika jijini Dar es salaam yamekuwa fursa muhimu ya kukutana na wachimbaji, wawekezaji na wawakilishi wa kampuni mbalimbali za migodi, hatua inayoweza kuongeza ushirikiano wa kibiashara na kupanua soko la bidhaa zake.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Masoko wa Superdoll, Godfrey Amos, alisema kampuni hiyo imekuwa ikishiriki maonesho mbalimbali kwa takribani mara tano hadi sita, lakini maonesho ya mwaka huu yamekuwa na tofauti kubwa kutokana na kushiriki kwa wadau wengi wenye mamlaka ya kufanya maamuzi ya ununuzi.
Alisema hali hiyo imeongeza matarajio ya kampuni kupata wateja wapya na kujenga mahusiano ya moja kwa moja na kampuni zinazohusika na shughuli za uchimbaji wa madini.
"Kwa mwaka huu tunashukuru sana kwa sababu tunaona watu wengi kutoka makampuni mbalimbali ambao wako katika ngazi za maamuzi. Hii ni tofauti na maonesho mengine ambayo wakati mwingine unakutana na watu ambao hawana mamlaka ya kufanya maamuzi ya ununuzi," alisema Amos.
Alisema Superdoll imekuwa ikitumia maonesho hayo kuonyesha bidhaa zake, hususan matairi makubwa ya mitambo inayotumika migodini, pamoja na vipuri vinavyohitajika katika shughuli za uchimbaji.
Alifafanua kuwa bidhaa hizo zinalenga kuhudumia wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa, ambao wanahitaji vifaa vya uhakika kwa ajili ya kuendesha mitambo yao na kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinaendelea.
Amos alisema katika maonesho hayo kampuni hiyo imeshirikiana na Teking ya China, wazalishaji wa matairi, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya sekta ya madini.
Katika hatua nyingine, Amos ameiomba Serikali kuendeleza maonesho na mikutano ya uwekezaji katika sekta ya madini kwa kuyasogeza katika mikoa mbalimbali inayozalisha madini, badala ya kuendelea kuyafanyia Dar es Salaam pekee.
Alitaja mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kusini kuwa miongoni mwa maeneo yanayopaswa kupewa nafasi ya kuandaa maonesho hayo ili kuwafikia wachimbaji na wafanyabiashara wengi zaidi.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia wadau ambao hushindwa kushiriki kutokana na umbali na gharama za safari kupata fursa ya kuonyesha bidhaa na huduma zao.
"Serikali iendelee kufanya maonesho kama haya, lakini yasiishie Dar es Salaam.
Yafanyike pia katika mikoa ambayo shughuli za madini zinafanyika ili kuwapa nafasi wadau wengi zaidi kushiriki," alisema.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma, Amos alisema Superdoll inaendelea kupanua mtandao wake wa biashara nchini ili kuwafikia wateja katika maeneo mbalimbali yenye shughuli za kiuchimbaji.
Alisema makao makuu ya kampuni hiyo yako Dar es Salaam, huku ikiwa na matawi Mwanza, Arusha na Dodoma, pamoja na mtandao wa wasambazaji katika mikoa ya Kusini, ikiwamo Songea.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea na maandalizi ya kufungua tawi jingine mkoani Tanga ili kuongeza wigo wa kuwahudumia wateja wake.
Alisema uwepo wa matawi katika maeneo mbalimbali unalenga kurahisisha upatikanaji wa matairi na vipuri kwa kampuni za migodi na wachimbaji, bila kulazimika kutegemea huduma kutoka Dar es Salaam pekee.
Ends..





إرسال تعليق