NESCH MINTECH GLOBAL YAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI MADINI KWA TEKNOLOJIA YA KISASA
.....Yasema wawekezaji sasa hawana sababu ya kusafirisha sampuli za madini kwenda Canada na Australia, huduma za upimaji zenye ithibati ya kimataifa zapatikana Mwanza; kampuni yatanua wigo hadi Saudi Arabia na Uingereza.
Na Joseph Ngilisho | DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Nesch Mintech Global imeibuka na suluhisho muhimu kwa wawekezaji na wachimbaji wa madini nchini kwa kutoa huduma za upimaji wa kitaalamu zinazowawezesha kubaini aina, kiwango na uwezekano wa kurejesha madini yaliyopo kwenye udongo na miamba kabla ya kuwekeza fedha katika shughuli za uchimbaji.
Hatua hiyo inalenga kupunguza hatari za uwekezaji, gharama za uendeshaji na changamoto ya kuendesha shughuli za uchimbaji bila kuwa na taarifa sahihi za kisayansi kuhusu rasilimali zilizopo katika eneo husika.
Mkurugenzi wa Nesch Mintech Global, Happiness Nesvinga, alisema hayo katika mkutano wa uwekezaji sekta ya madini,jijini Dar es salaam,ambapo kampuni hiyo imejikita katika kuhakikisha wawekezaji na wafanyabiashara wa madini wanapata taarifa sahihi za kitaalamu zinazowawezesha kufanya maamuzi yenye tija katika mnyororo mzima wa shughuli za madini.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya wawekezaji ni kuanza uchimbaji au uchakataji bila kuelewa kwa kina kiwango cha madini kilichopo ardhini na kiasi kinachoweza kupatikana baada ya kuyachakata.
Alieleza kuwa kampuni hiyo inatoa huduma za vipimo maalumu vya kisayansi vinavyosaidia kutatua changamoto hiyo, ikiwemo Geochemical Analysis, ambacho hubaini aina na kiwango cha madini kilichopo katika kila tani ya udongo au miamba.
Pia kuna kipimo cha Metallurgical Test, kinachobainisha kiwango cha madini kinachoweza kurejeshwa kutoka kwenye sampuli husika kupitia teknolojia mbalimbali za uchakataji.
Pia kuna kipimo cha Metallurgical Test, kinachobainisha kiwango cha madini kinachoweza kurejeshwa kutoka kwenye sampuli husika kupitia teknolojia mbalimbali za uchakataji.
Nesvinga alisema vipimo hivyo ni muhimu kwa kuwa vinamsaidia mwekezaji kujua siyo tu kiasi cha madini kilichopo ardhini, bali pia uwezo wa kuyatoa na teknolojia inayoweza kutumika kupata matokeo bora kiuchumi.
Huenda ukawa na eneo lenye madini, lakini usipofanya vipimo sahihi huwezi kujua kiwango chake wala kiasi unachoweza kukipata baada ya uchakataji. Sisi tunamsaidia mwekezaji kupata majibu hayo kabla hajaingia kwenye uwekezaji mkubwa," alisema.
Alisema baada ya kupata matokeo ya vipimo, kampuni hiyo hutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu aina ya mitambo na teknolojia inayofaa kutumika kulingana na sifa za madini yaliyobainika.
Alitaja teknolojia hizo kuwa ni Carbon in Pulp (CIP), Vat Leaching na Heap Leaching, ambazo huchaguliwa kulingana na matokeo ya vipimo na uwezo wa kiufundi wa madini husika.
Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia sahihi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha wachimbaji wanaongeza ufanisi, wanapunguza gharama zisizo za lazima na kupata manufaa makubwa kutokana na rasilimali wanazozalisha.
MAABARA YA TANZANIA YAPUNGUZA GHARAMA ZA WAWEKEZAJI
Katika hatua nyingine, Nesvinga alisema kampuni hiyo imekuwa sehemu ya suluhisho kwa wawekezaji waliokuwa na utaratibu wa kusafirisha sampuli za madini kwenda nchi za Canada na Australia kwa ajili ya vipimo, hali iliyokuwa ikiongeza gharama na kuchelewesha upatikanaji wa majibu.
Alisema Nesch Mintech Global ina maabara iliyopo Mwanza yenye ithibati ya kimataifa (International Accreditation), inayowezesha huduma za upimaji kutolewa nchini kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.
Alisema uwepo wa huduma hizo nchini ni fursa kubwa kwa wawekezaji kwa kuwa wanapata huduma karibu zaidi, wanapunguza gharama za usafirishaji wa sampuli na wanaokoa muda wa utekelezaji wa shughuli zao.
Ends

إرسال تعليق