ARUSHA DC YAKWAMA KUPANDISHWA HADHI, RCC YAKATAA MAPENDEKEZO
...Makalla ataka mchakato urudiwe upya, Ngorongoro kutaka kugawanywa kuwa halmashauri mbili kutokana na umbali wa kilometa 400
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) imekwama katika mpango wa kupandishwa hadhi na kuwa Manispaa baada ya Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kukataa kupokea mapendekezo hayo, kikieleza kuwa bado hayajakamilisha taratibu zinazotakiwa kisheria na kiutawala.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha RCC Mkoa wa Arusha, ambapo wajumbe walieleza kuwa baadhi ya vikao vya kisheria na kiutawala vinavyopaswa kujadili na kupitisha mapendekezo hayo bado havijakaa, hivyo kuagiza hoja hiyo irudishwe kwa ajili ya kufanyiwa mapitio na kukamilisha taratibu zilizobaki.
Akizungumza Nov 14,2026 katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, alisema suala la kubadilisha hadhi ya halmashauri linahitaji uchambuzi wa kina wa wataalamu na kuzingatia matokeo yake kwa wananchi, ikiwamo mabadiliko ya kiutawala na mfumo wa makazi.
Makalla alitahadharisha kuwa kupandishwa hadhi kwa eneo hilo na kuwa Manispaa kutakuwa na athari kwa mfumo wa vijiji, hivyo ni muhimu halmashauri hiyo kupitia upya mchakato mzima kabla ya kuwasilisha mapendekezo yake.
Alisema Serikali Kuu haina kikwazo kwa Halmashauri ya Arusha kupandishwa hadhi na kuwa Manispaa kama ilivyoomba, lakini lazima taratibu zote zinazotakiwa zikamilishwe.
Hoja hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu namna ya kupanga upya maeneo ya kiutawala mkoani Arusha ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hasa katika maeneo yenye changamoto za umbali na jiografia.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro alisema halmashauri hiyo inajiandaa kuwasilisha pendekezo la kugawanywa na kuanzisha halmashauri mbili kutokana na ukubwa wa eneo lake na ugumu wa jiografia unaokwamisha utoaji wa huduma.
Alisema baadhi ya wananchi wanaishi umbali wa zaidi ya kilometa 400 kutoka makao makuu ya halmashauri, hali inayosababisha gharama kubwa za usafiri na kuchelewesha upatikanaji wa huduma za kiutawala.
Alisema halmashauri hiyo yenye kata 38 itafanya utafiti wa kina na kuandaa hoja itakayowasilishwa katika kikao kijacho ili kuonyesha umuhimu wa kugawanywa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
Alisema baadhi ya madiwani hulazimika kutumia siku nzima kusafiri hadi makao makuu ya halmashauri na kulazimika kulala kabla ya kushiriki kikao siku inayofuata, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji.
NCAA YALALAMIWA KUKWAMISHA MAPATO
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, ameiomba Serikali ya Mkoa wa Arusha kuingilia kati mkwamo wa muda mrefu wa mapato yanayotokana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), akisema hali hiyo inaathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Ndoinyo alisema halmashauri inahitaji mapato hayo ili kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, hivyo akamwomba Mkuu wa Mkoa kutumia nafasi yake kusaidia kuondoa changamoto hiyo.
Pia alitumia kikao hicho kuibua hoja ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Wasso, akisema eneo lililopendekezwa limefanyiwa utafiti na kuonekana linafaa kwa ajili ya mradi huo.
Alisema halmashauri hiyo tayari ilishawasilisha ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu ujenzi wa uwanja huo, hivyo akawaomba wajumbe wa RCC kuunga mkono wazo hilo ili kuharakisha utekelezaji wake.
LONGIDO YATAKA SHULE ZA BWENI, KITUO CHA UMEME
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido alipendekeza kujengwa kwa shule mbili za sekondari za bweni katika kila tarafa ili kukabiliana na changamoto ya mahudhurio ya wanafunzi, inayochangiwa na mfumo wa maisha ya wafugaji wanaohama kutoka eneo moja kwenda jingine.Alisema mazingira hayo yanaathiri mwendelezo wa masomo kwa watoto, hivyo shule za bweni zitasaidia kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kuendelea na elimu bila kukatizwa na kuhama kwa familia zao.
Kuhusu changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, alisema halmashauri imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 10 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo katika wilaya hiyo na maeneo mengine yenye changamoto zinazofanana.
VYAMA RAFIKI VYATAKIWA KUSHIRIKISHWA
Katika kikao hicho, Makalla aliwaagiza wakuu wa wilaya kushirikishwa katika vikao vya Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC), huku akisisitiza maoni yao yazingatiwe katika mijadala na maamuzi yanayohusu maendeleo ya maeneo yao.
Agizo hilo lilifuatia hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Makini Mkoa wa Arusha, Simon Paulo Ngilisho, aliyesema vyama rafiki vya siasa havijashirikishwa ipasavyo katika vikao vya DCC.
Aidha, Makalla alitoa maelekezo kuhusu usajili wa vikundi vinavyolenga kunufaika na mikopo ya fedha za serikali, akitaka kuhakikisha hakuna vikundi hewa vinavyosajiliwa na kupewa nafasi ya kunufaika na fedha hizo.
Aliwaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanathibitisha uhalisia wa vikundi kabla ya kuvisajili, huku taarifa za usajili na fursa za mikopo zikitolewa kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara na vyombo vya habari.
Alisema hatua hiyo itasaidia wananchi kupata taarifa sahihi na kufahamu fursa zilizopo badala ya kuachwa nje ya huduma zinazotolewa na serikali.
Akiahirisha kikao hicho, Makalla pia alisema mkoa umejipanga kuwa na timu ya mpira wa miguu itakayowakilisha Mkoa wa Arusha, ambayo inaweza kuundwa kupitia halmashauri au taasisi zilizopo mkoani humo.
Ends









Post a Comment