ST PATRICK YAFUFUA MOUNT MERU MARATHON, SIMBU ATAKA KUREJEA KILELENI KIMATAIFA
...Waandaaji watangaza mbio za kilometa 21, 10, tano na 2.5, wakilenga kuwashirikisha watoto, wazee na wanariadha wa mataifa mbalimbali
Na Joseph Ngilisho | Arusha
MASHINDANO ya Mount Meru Marathon yanatarajiwa kurejesha makali yake katika ramani ya riadha nchini na kimataifa baada ya Shule ya St Patrick kupitia taasisi ya Trust kuanzisha upya mpango wa kuyaendeleza mashindano hayo ya kihistoria, huku bingwa wa dunia wa marathon mwaka 2025, Alphonce Simbu, akitaka yawe jukwaa la ushindani wa kimataifa na kukuza vipaji vya vijana.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 6, 2026, katika viwanja vya General Tyre jijini Arusha, yakiwa na mbio za kilometa 21, 10, tano na 2.5, zitakazotoa nafasi kwa makundi mbalimbali ya washiriki, wakiwemo watoto na wazee.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo, Simbu alisema Mount Meru Marathon ina historia kubwa katika maendeleo ya riadha nchini na iliwahi kuwa miongoni mwa mashindano yaliyovutia wanariadha wenye majina makubwa kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema alipofika Arusha kwa mara ya kwanza mwaka 2006, alikuwa akisikia historia ya mashindano hayo na jinsi yalivyokuwa yakitumiwa na wanariadha wakubwa kupima uwezo wao kabla ya kushiriki mashindano mengine ya kimataifa.
Hata hivyo, alisema baadaye mashindano hayo yalipoteza mwendelezo wake, hivyo juhudi za kuyafufua ni hatua muhimu katika kurejesha hadhi yake na kulitangaza jina la Arusha kupitia michezo.
Ninakupongeza mkurugenzi pamoja na timu yako kwa uamuzi wa kufufua Mount Meru Marathon. Hizi ni mbio zilizokuwa na historia kubwa na jina lake lilisikika sana kutokana na ushindani uliokuwepo na wanariadha wakubwa waliokuwa wakishiriki,” alisema Simbu.
Alisema ili mashindano hayo yarudi katika hadhi yake ya awali, ni muhimu kuimarisha ubora wa maandalizi na kuwashirikisha wanariadha wa kimataifa, hatua itakayoongeza ushindani na kutoa fursa kwa wanariadha wa Tanzania kupima viwango vyao dhidi ya wakimbiaji wenye uzoefu mkubwa.
Simbu pia alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kundi la watoto, akisema maendeleo ya riadha yanapaswa kuanzia katika umri mdogo ili kujenga kizazi chenye mwamko wa michezo.
Alisema watoto wanapaswa kufundishwa kuwa riadha si burudani pekee, bali pia ni njia ya kuimarisha afya, kukuza vipaji na kujipatia fursa za ajira na kiuchumi.
Ukitaka jambo zuri liendelee na kuwa kubwa zaidi, ni lazima ulipandikize kwa watoto. Tukiwajenga kuanzia sasa na kuwaeleza kuwa riadha ina faida katika afya, uchumi na ajira, tutajenga kizazi chenye mwamko mkubwa wa michezo,” alisema.
Aidha, alisema Mount Meru Marathon ina nafasi ya kuunganisha riadha na utalii, kutokana na Arusha kuwa na vivutio muhimu ikiwemo Mlima Meru na hifadhi za wanyamapori.
Alisema mashindano hayo yanaweza kuvutia washiriki na wageni kutoka mataifa mbalimbali ambao watapata fursa ya kutembelea vivutio hivyo, hali itakayochochea shughuli za hoteli, usafiri, biashara na sekta nyingine za huduma.
Alishauri waandaaji kufanya kazi kwa karibu na Shirikisho la Riadha Tanzania ili kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa kuzingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa kimataifa.
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Rogat John Steven Akwary, alisema shirikisho hilo limejipanga kushirikiana na waandaaji kurejesha hadhi ya Mount Meru Marathon.
Akwary alisema mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 1984 yalikuwa yakivutia wanariadha kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo Kenya, Ethiopia, Djibouti, Eritrea na Ujerumani.
Alisema katika miaka hiyo, mashindano hayo yalikuwa na mfumo wa kuwashirikisha wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari, huku halmashauri mbalimbali zikisaidia kupata na kusafirisha wanafunzi waliofanya vizuri katika riadha.
Alisema utaratibu huo ulisaidia kutoa fursa kwa wanariadha chipukizi kukutana na wakimbiaji wenye uzoefu, hivyo kuchochea ukuaji wa vipaji na ushindani.
Alisema mwaka huu waandaaji wamepanua wigo wa ushiriki kwa kuweka mbio za kilometa 2.5 kwa watoto kuanzia miaka mitano, huku wakilenga pia kuwashirikisha wazee ili kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa mazoezi katika kila hatua ya maisha.
Dkt Mosha alisema dhamira yao ni kuhakikisha watu wa rika mbalimbali wanapata nafasi ya kushiriki, akisisitiza kuwa mazoezi ni sehemu muhimu ya kujenga afya na michezo inaweza kuwa chanzo cha ajira.
Alieleza kuwa alikabidhiwa jukumu la kuongoza mashindano hayo mwaka 2020, lakini mipango ya kuyaendeleza iliathiriwa na janga la UVIKO-19, lililosababisha shughuli hizo kutofanyika hadi mwaka 2023.
Alisema mwaka 2024 mashindano hayo yalirejea na kufanikiwa kuvutia washiriki zaidi ya 2,000, hatua aliyoitaja kuwa msingi wa kuendelea kuyafufua.
Aliongeza kuwa mashindano yaliyopangwa kufanyika Novemba 3, 2025, yalilazimika kuahirishwa kutokana na changamoto zilizojitokeza na sasa yamepangiwa kufanyika Desemba 6, 2026.
Dkt Mosha aliwataka wanariadha, wananchi, taasisi na wadau wa michezo kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo, akisema lengo ni kulifanya Mount Meru Marathon kuwa jukwaa la kukuza riadha, utalii na uchumi wa jamii.
Ends









Post a Comment